Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Mbeya wahaha na mgawo wa maji

Mgao Wa Maji ,Mbeya Wananchi Mbeya wahaha na mgawo wa maji

Mon, 10 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakati wakazi wa kata za Ilemi, Isanga na Sinde jijini Mbeya wakilia na ukosefu wa maji kwa siku nane sasa, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Mbeya Wssa) imesema maeneo hayo yote kwa sasa yanapata maji kwa mgawo.

Asilimia kubwa ya wakazi wa kata hizo sasa wanategemea maji ya visima ambayo si salama kwa afya.

Maeneo hayo yanalishwa na chanzo kimoja cha maji cha Mwafrika kilichopo Mtaa wa Ilolo, hali inayokwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 10 2024, baadhi ya wananchi wamesema hali imekuwa mbaya kwa sababu hata baadhi ya shughuli zao za kiuchumi zimekwama kutokana na ukosefu wa maji.

Victor John, mkazi wa Mtaa wa Makunguru jijini humo, amesema inampa wakati mgumu kuendelea na biashara ra mgahawa kwa kuwa maji mengi si salama.

“Sisi baba lishe ndio tunapata wakati mgumu, maji ni shida, tutatumiaje maji ya visima ambayo si salama kwa binadamu?” amehoji na kuomba mamlaka kulifanyia kazi.

Kwa upande wake, Janeth Mlanzi amesema hivi sasa wanalazimika kuamka alfajiri kuwahi foleni katika chanzo cha maji Mwafrika, vinginevyo yanakuwa yamechafuka.

“Maji ndio uhai wa kila mmoja, tunaamka mapema kuwahi foleni, watoto wamefunga shule lakini hawapumziki tunadamka nao kusaka maji na hatujui huduma itarejea lini,” amesema Janeth.

Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa mamlaka hiyo, Neema Stanton amesema maeneo hayo yote kwa sasa yanapata maji kwa mgawo.

Amesema ni ngumu kujua huduma hiyo itarejea lini kwa sababu mafundi bado wanaendelea na ukarabati wa miundombinu, ikiwamo kufunga mabomba.

“Siwezi kusema ni lini kwa sababu kuna sehemu wanatengeneza barabara, mfano kule Mwenge bomba limekatwa na hakuna maji kwa zaidi ya siku hizo, japo tuliagiza vifaa vipya nitafuatilia kama vimefika,” amesema.

Amesema licha ya maeneo mengi kukosa maji kutokana na mgawo uliosababishwa na matengenezo makubwa ya miundombinu, atafuatilia kuhakikisha wananchi wanarejeshewa huduma hiyo haraka.

Hata hivyo, Juni mosi, 2024, Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson akiwa katika mkutano wa hadhara Bonde la Uyole, alitahadharisha wananchi kwamba huenda kukawa na mgawo wa maji kutokana na kiangazi.

“Inapofika kiangazi changamoto huwa kubwa na kusababisha mgawo, lakini Serikali imetuletea Sh117 bilioni za kumaliza mradi wa maji kutoka Mto Kiwira ambao utamaliza tatizo hili,” alisema Dk Tulia.

Chanzo: Mwananchi