Kigoma. Serikali imetenga Sh722milioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wa kijiji cha Kidahwe mkoani Kigoma ili kupisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Machi 26, 2019 na Waziri wa Nishati, Medard Kalemani wakati akikagua eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, akibainisha kuwa umeme huo utatokea mkoani Tabora.
Amesema kabla ujenzi haujaanza katika eneo hilo lazima wananchi hao watalipwa fidia zao kwani wameshafanya makadirio na kufikia Aprili au Juni 2020, mkoa huo utakuwa na umeme wa kudumu.
"Kuna wananchi walikuwa wanamiliki eneo hili na wana haki zao kabisa za msingi, na kabla ujenzi haujaanza lazima wananchi hao wafidiwe kwanza ndio ujenzi uendelee," amesema Waziri Kalemani.
Waziri Kalemani amesema suala la fidia lina mambo mengi ni lazima wajiridhishe kwa kila mmoja mwenye eneo lake ndio waweze kuwalipa bila kuwa na mkanganyiko.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kidahwe, Shaban Edward amemuomba waziri kuhakikisha malipo hayo hayachelewi kwani kuna wananchi katika eneo hilo walilima mazao yao ya biashara.
Amesema Serikali ikiwalipa mapema wananchi hao watakuwa na fedha za kwenda kununua aneo lingine na kulima mazao yao kama ilivyokuwa awali.
Eneo hilo lenye jumla ya ekari 448 na wananchi katika kijiji hicho watakaolipwa fidia hiyo ni 416.