Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Iringa watakiwa kuchangamkia fursa za utalii

Sun, 22 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Wakazi wa Iringa na  Mikoa jirani wametakiwa kuchangamkia  fursa za utalii  zilizoanza kutangazwa kwenye maeneo yao ili wajikwamue kiuchumi.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa kiwanda cha Qwihaya  cha nguzo za umeme mjini Mafinga, Leonard Mahenda wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda lake katika maonyesho ya utalii wa kusini yanayoendelea mjini Iringa.

Amesema kuna fursa nyingi zinazotokana na utalii ambazo kama watazitumia ipasavyo zinaweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Ameipongeza Serikali kwa kuanzisha mkakati wa kutangaza vivutio vya utalii kwenye Mikoa hiyo kwa sababu vingi havikuwa vikijulikana licha ya kuwa vinaweza kuchangia kukua kwa Pato la Taifa.

Amesema kampuni hiyo imeweka banda la maonyesho kwenye maadhimisho hayo kwa sababu kuna uhusiano mkubwa kati ya mazao ya misitu na utalii.

“Tumeamua kutumia vizuri fursa ya maonyesho kwa sababu bidhaa za misitu zinahamasisha utalii, sio tu kwamba zinaweza kutumika kwenye ujenzi wa hoteli na vitu vingine lakini zinahamasisha pia utunzaji wa mazingira,” amesema Mahenda.

Pia Soma

Advertisement
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Iringa, Enock Ugulumo amesema bado inahitajika nguvu zaidi kutangaza vivutio hivyo ili watalii waanze kumiminika kama wanavyojitokeza kwenye Mikoa ya Kaskazini.

“Tunaweza kufikia ndoto ya kuwa kitovu cha utalii kama kila mtu atashiriki kutangaza vivutio hivi, binafsi nimefarijika kuona maonyesho ya aina hii kwenye mikoa yetu niombe tu mkakati huu usiwe zimamoto,” amesema Ugulumo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati amesema ukuaji wa sekta ya utalii kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini ndio nguvu ya kukua kwa viwanda na ajira kwa wananchi ikiwa itatumika vizuri.

Utalii wa Nyanda za Juu kusini unaundwa na Mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, KatavI, Morogoro, Songwe na Rukwa.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz