Mbulu . Mradi mkubwa wa maji Getanyamba uliowezeshwa na 4CCP, wenye thamani ya Sh61.9 milioni umezinduliwa na Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Getanyamba wilayani Mbulu mkoani Manyara na kuondoa changamoto ya huduma hiyo kwa wakazi wa eneo hilo.
Mratibu wa kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP), Eliminata Awet akizungumza Juni 15, 2019, amesema mradi huo umefanikishwa na Norwegian Church Aid (NCA) kwa Sh51.9 milioni huku wananchi wakichangia nguvu zao zilizothaminishwa kwa Sh10 milioni.
Amesema mradi huo utawanufaisha wakazi 1,000 pekee kwenye kijiji hicho chenye wakazi 4,250 hivyo wengine 3,250 bado wataendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji.
“Mradi huu utawanufaisha wananchi hao ambao walikuwa wanachota maji korongoni kwa kutembea umbali wa kilomita moja hadi tatu ambayo hayakuwa safi wala salama,” amesema Awet.
Kiongozi wa mbio za Mwenge, Mzee Mkongea Ally akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, amepongeza juhudi za wakazi wa eneo hilo kwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha mradi huo.