Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Gairo watembea kilomita 134 kusaka huduma ya mahakama

Wananchi Gairo watembea kilomita 134 kusaka huduma ya mahakama

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wananchi wa Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wanatembea kilomita 134 kufuata huduma ya mahakama katika Wilaya ya Kilosa.

Imeelezwa kuwa umbali huo unasababisha kesi za watoto waliopewa mimba kutotatuliwa.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 20, 2019 na mkuu wa Wilaya ya Gairo, Seriel Mchemba mbele ya Rais John Magufuli aliyekuwa njiani kwenda Dodoma.

Mkuu huyo wa Wilaya mbali na kudai mahakama, pia aliomba ufanyike ujenzi wa ofisi mkuu wa wilaya, kutatuliwa kwa kero ya maji pamoja na ujenzi wa stendi.

Seriel amesema kukosekana kwa mahakama hiyo kesi nyingi za watoto kupewa mimba zimeshindwa kutatuliwa kutokana na gharama za usafiri.

“Wanaotoa ushahidi katika kesi hizo wanashindwa  kwenda kutokana na gharama jambo linalosababisha kesi nyingi kutoendelea.”

“Mimi sina ofisi ila nimejishikiza katika mamlaka ya mji mdogo, ofisi ni ndogo sana huku DAS (Katibu tawala) akichangia ofisi na maofisa tarafa katika ofisi ndogo,” amesema Seriel.

Amesema wamepokea mradi wa maji wa Sh6.6 bilioni sambamba na Sh2 bilioni za mtambo wa kuchuja maji ya chumvi na waliahidiwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuwa Novemba 15, 2019 maji yangetoka lakini imekuwa tofauti.

Akijibu suala la mahakama, Rais Magufuli ameahidi kulifanyia kazi.

“Ni vyema tuwe na mahakama ya wilaya hapa kwa sababu watu wa Gairo wanapelekwa sana mahakamani. Nitawasaidia, nitakwenda kuzungumza na jaji mkuu pamoja na jaji kiongozi tuone namna ya kuanza kujenga mahakama hapa Gairo,” amesema Rais Magufuli.

Kuhusu stendi aliwataka kuanza kutumia fedha kidogo zinazokusanywa na Halmashauri kuliko kusubiri kujengewa na Serikali.

“Haiwezekani halmashauri zaidi ya 180 zijengewe stendi na Serikali lakini nimeielewa, mmeshindwa hata kujenga kibanda hapa. Halmashauri  hii yote mmeshindwa kujenga hata banda la Sh10 milioni kwa ajili ya kupumzika wasafiri. Mambo mengine ni ninyi mnatakiwa kufanya mnasubiri Magufuli aje awajengee.”

“Mambo mengine ni mipango yenu. Diwani wa hapa aliomba stendi wakati yeye alipitisha soko, RC (mkuu wa Mkoa), DC (mkuu wa Wilaya) tengeni fedha kwenye mapato yenu mjenge stendi,” amesema Magufuli.

Akizungumzia maji, Magufuli aliomba kufuatilia suala hilo kwa Profesa Mbarawa na kuwapa mrejesho kwa maelezo kuwa anataka kujua kitu gani kimekwamisha mradi kuanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz