Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Dar walalamikia ratiba mgawo wa maji

MRADI MAJI Wananchi Dar walalamikia ratiba mgawo wa maji

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mgawo wa maji katika Jiji la Dar es Salaam umeendelea kuwa maumivu kwa wananchi wanaodai Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imeshindwa kusimamia ratiba ya mgawo huo.

Mgawo wa maji ulianza Oktoba 27 hadi 31 katika maeneo yanayohudumiwa na mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, huduma hiyo ilikuwa inapatikana na kukosekana kwa saa 24 na pengine saa 12.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ndiye aliyetangaza kuanza kwa mgawo huo baada ya kutembelea vyanzo hivyo vya maji Oktoba 25 akisema sababu ni kupunguza kwa uzalishaji wa maji unaotokana na ukame.

“Uzalishaji umepungua kutoka lita za ujazo milioni 466 kwa siku hadi kufika lita milioni 300 sawa na asilimia 64 ya uzalishaji wote wa maji,” alisema.

Kwa mujibu wa Dawasa, maji yanayohitajika Dar es Salaam kwa siku ni lita milioni 500, hivyo kufanya kuwa na uhaba wa lita 200 kwa sasa. Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshaoa taarifa ikieleza mvua za Novemba mwaka huu hadi Aprili mwakani zitanyesha chini ya wastani katika mikoa 14, hivyo kusababisha ukame katika maeneo hayo.

Baada ya Dawasa kutoa ratiba ya mgawo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alipotembelea ujenzi wa bomba la maji safi la Dawasa, lililopo Tegeta Wazo, aliitaka mamlaka hiyo kuhakikisha wanazingatia ratiba za mgawo walioutangaza. “Ratiba ya mgawo wa maji ni muhimu ifuatwe bila upendeleo,” alisema Aweso,

Hata hivyo, hilo limekuwa tofauti katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam ambapo wananchi wamekuwa wakiilalamikia Dawasa kwa kushindwa kuzingatia ratiba.

“Hatuna tatizo na mgawo, tumekubali, lakini kwa nini ratiba tuliyotangaziwa haifuatwi? Toka Alhamisi mpaka leo (jana, saa 9 alasiri) hakuna maji, hakuna taarifa nini tena kimetokea,” alisema Mary Frank, Mkazi wa Mbezi Beach. Hoja inayoungwa mkono na Norbert Siwale, Mkazi wa Golani aliyesema licha ya Dawasa kutozingatia ratiba yao wamekuwa na haraka ya kuwatumia bili ya maji kitu ambacho ni uonevu.

Malalamiko kama hayo yameripotiwa na wananchi wa maeneo ya Kinondoni, Tabata, Ilala, Mikocheni, Buguruni, Kimara, Mbezi na Mbweni huku meneja mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro alipotafutwa na gazeti hili kuhusu suala hilo alikiri kupokea malalamiko hayo akisema mamlaka inajipanga kutolea ufafanuzi kwa umma sababu iliyochangia kujitokeza kwa changamoto hiyo.

Chanzo: mwanachidigital