Wananchi wa Kijiji cha Mwai, wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro wanaishi kwa kutokuwa na mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama, nishati ya umeme na kutokuwa na mawasiliano ya simu.
Wananchi hao hulazimika kutumia maji ya madimbwi, kupanda juu ya miti kutafuta mawasiliano ya simu kutokana na kutokuwa na mtandao wa mawasiliano na kukosekana kwa nishati muhimu ya umeme.
Wakizungumza jana kijijini hapo mmoja wa wananchi hao Elisei Basil, alisema wanapotaka kuwasiliana na ndugu zao kwa simu hulazimika kwenda kijiji cha jirani au eneo la mlimani, kupanda kwenye miti ili kupata mawasiliano.
"Nilihamia kijijini hapa mwaka 1974, hadi leo hii hatujawahi kupata umeme wala maji safi na salama na tunalazimika kutumia maji ya kwenye madimbwi hali ambayo inapeleka kuugua homa za matumbo pamoja na kuhara," alisema.
Alisema kijiji hicho kina shule zahanati makanisa ya madhebu yote lakini kimetengwa na Serikali kwa kutowapatia huduma muhimu za kibinadamu.
Ofisa mtendaji wa kijij hicho, Juma Jackson, alisema kijiji kinakabiliwa na ukosefu wa umeme na maji safi na salama na kwamba ili awasiliane na viongozi wake, hutembea zaidi ya kilometa 12 kwenda kijiji cha jirani, akapige simu ndipo arudi ofisini kwa ajili majukumu mengine ya kikazi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa zahanati ya kijiji hicho, Jastas Juma, alisema kukosekana kwa umeme kunasababisha majokofu ya zahanati kushindwa kuhifadhi chanjo na dawa zinazohitajiwa.
Alisema kijiji hicho kimekuwa na magonjwa ya tumbo na mlipuko mara kwa mara kutokana na kukosekana kwa maji safi na salama.
Dk Juma, alisema zahanati hiyo imefungwa umeme wa jua, lakini hauna uwezo wa kuendesha makokofu hayo.
Naye mdau wa maendeleo, Ewald Kilasara, alisema alilazimika kupeleka maji safi na salama katika zahanati na shule ya msingi kutokana na kuwepo kwa magonjwa ya milipuko.
Alisema nguzo za umeme zilipelekwa kijijini hapo zaidi ya miaka saba na mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya alisema wako mbioni kupeleka huduma hizo muhimu.