Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanakijiji wachoma misitu

6a977f924153092864ef443d41f4f104.png Wanakijiji wachoma misitu

Wed, 29 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BAADHI ya wananchi wa Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga wamedaiwa kuvamia na kuchoma misitu katika Kituo cha kufundishia cha Kizumbi kilichopo chini ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Mucos).

Mratibu wa kituo hicho, Grace Maleko aliyasema hayo juzi wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha wajumbe wa baraza la chuo hicho ambapo alisema wanakijiji wamekuwa wakivamia maeneo kwa kukata miti na kuchoma moto.

Maleko alieleza kuwa changamoto hizo zinatokana na eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 107 kutokuwa na uzio, hivyo wanakijiji wanatumia fursa hiyo kufanya uvamizi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama kutokana na uchomaji wa moto unaofanywa wakati wakitafuta kuni.

“Tunazo changamoto nyingi kwenye kituo chetu ukiwemo ubovu wa barabara za kuingia na kutoka ndani ya kituo, kutokuwepo kwa kisima cha maji ya chini kwa matumizi ya kawaida na migogoro ya uvamizi ya wanakijiji ya kulima, kuchungia mifugo na kukata miti,” alisema Maleko.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi, Profesa Alfred Sife alisema wana mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kituo hicho chenye hekta 107.

Eneo hilo lina hati miliki na kwa kushirikiana na serikali wanaamini watamaliza tatizo hilo.

Profesa Sife alisema baada ya kuwa Chuo Kikuu Moshi mwaka 2014 wanaendelea kujipanga na kwa sasa mabadiliko makubwa yameanza kuonekana ambapo kwa sasa kituo kina wanafunzi 531 kwa mwaka wa masomo 2019/2020.

Mwenyekiti wa Baraza la chuo, George Yambesi aliwataka kuendelea kuitunza miti ya asili ili iendelee kuwa kivutio kikubwa kwenye chuo hicho na kusisitiza kuwa uvamizi unaofanyika usije kuwa chanzo cha kumaliza miti hiyo na kusisitiza kuendelea kufuatilia.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha, Profesa Fredy Kilima alisema watahakikisha kituo hicho kinaendelea kuboreshwa ili kuondoa tofauti kati ya chuo cha Ushirika Moshi na Kituo cha Kizumbi ili mwanafunzi anayepangiwa Kizumbi na anayekwenda Moshi asione tofauti.

Chanzo: habarileo.co.tz