Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanakijiji kuona maji safi mara ya kwanza

43842 Pic+maji Wanakijiji kuona maji safi mara ya kwanza

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chamwino. Kaya zaidi ya 750 katika kijiji cha Msamalo wilaya ya Chamwino kwa mara ya kwanza watu wake wataanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama tangu kuanzishwa kwa kijiji chao baada ya mitambo ya kuchimba visima kupelekwa

Msamalo ni moja ya vijiji vyenye maendeleo katika wilaya ya Chamwino lakini hakina maji safi na salama kwa muda mrefu jambo lililopelekea hivi karibuni wananchi kupeleka kilio chao hicho kwa waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi baada ya kumtumia barua waziri wake, Seleman Jafo na kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha wananchi na mifugo namna wanavyopata shida.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, mbunge wa Chilonwa, Joel Mwaka na mhandisi wa maji wa wilaya hiyo, Godfrey Mbabaye walitembelea eneo hilo na kuahidi maji yataanza kuchimbwa ndani ya siku tatu.

Wakati wa ziara hiyo wajumbe wa Serikali ya kijiji walisema hali ni mbaya katika eneo hilo kwani wananchi wanakunywa maji machafu.

Mjumbe wa Serikali ya kijiji, Timoth Mdobochi alisema kumekuwa na danadana ya muda mrefu kwa viongozi kushindwa kutekeleza ahadi zao hata kuwafanya wananchi kukata tamaa.

Jana diwani wa kata ya Msamalo, Elias Kaweya alithibitisha wataalamu wameshaweka kambi katika eneo hilo na mitambo imefungwa tayari kwa kazi ya kuchimba kisima ambacho alisema kitakuwa na maji mengi ya kutosha vijiji viwili.

“Mitambo imeletwa na kazi imeshaanza, ni imani yetu sasa kilio chetu kitafika mwisho na mimi kwenye vikao vya mabaraza nitapumua kwani nilishakosa ajenda nyingine zaidi ya maji Msamalo,” alisema Kaweya

Mhadishi wa maji, Godfrey Mbabaye alisema maandalizi yote kwa ajili ya kazi hiyo yamekamilika hivyo haitawachukua muda wananchi wataanza kutumia maji safi na salama.



Chanzo: mwananchi.co.tz