Wakazi wa Kitongoji cha Mwikoko katika Kijiji cha Chitare Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini wameiomba Serikali kusajili shule shikizi iliyopo katika kitongoji hicho, kuwa shule ya msingi ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kutoka katika eneo hilo kwenda shule ya Msingi Chitare B kwaajili ya masomo.
Ombi hilo wamelitoa baada ya kupokea shilingi milioni 60 kwaajili ya ujenzi wa madarasa matatu kupitia fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Serikali ambapo wameomba usajili huo ufanyike ili mwakani wanafunzi waweze kuendelea na masomo katika shule hiyo.
Wakizungumza na Kaimu Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo ,Tereza Patrick wakaazi hao wamesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa madarasa matatu shule hiyo itakuwa na jumla ya madarasa saba na ofisi moja ya walimu.
Mwenyekiti wa kitingoji hicho, Athumani Matembele amesema baada ya wakazi wa eneo hilo kuona adha wanayoipata watoto wao ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kwenda shule mama ya kijiji hicho kwa pamoja walimua kuanza ujenzi wa shule shikizi.
"Kwa pamoja tuliamua kuanza ujenzi wa shule shikizi hapa kwenye kitongoji chetu ambapo tulipata msaada kutoka kwa mbunge wetu Sospeter Muhongo aliyetuchangia mifuko 180 ya saruji, mabati 80 na tukaweza kujenga vyumba vinne pamoja na ofisi kwahiyo haya madarasa mengine matatu yakikamilika tunaomba tupewe shule kamili" amesema
Amesema kuwa pamoja na kupokea kiasi hicho cha fedha wakazi wa kitongoji hicho wamekubaliana kuchangia viashiria kwaajili ya ujenzi huo ili fedha hizo ikiwezekana ziweze kujenga madarasa zaidi ya matatu kama ambavyo imekusudiwa.
Msimamizi wa shule hiyo, Mwalimu Richard Mambo amesema kuwa shule hiyo yenye darasa la awali hadi la pili ina jumla ya wanafunzi 250 ambao wanatoka katika kitongoji hicho pamoja na kitongoji cha jirani cha Kasia.
Amesema kuwa endapo shule hiyo itasajiliwa na kuwa shule kamili anaamini kuwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi katika eneo hilo itaongzeka kwani upo uwezekano mkubwa kwa watoto wengi kushindwa kupata elimu kutokana na umbali uliopo na ikilinganishwa na umri wao.
Kaimu Afisa Elimu Msingi wa Halmashuri ya Musoma Vijijini, Tereza Patrick, mbali na kuwapongeza wakaazi hao kwa kujitolea kufanikisha ujenzi wa madarasa manne ya awali, amesema serikali inakwenda kushugulikia ombi hilo na kuangalia namna litakavyotekelezwa.
Amesema kuwa serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya elimu ili kuongeza ufaulu na ubora wa taaluma nchini hivyo wakazi hao wanapaswa kuungwa mkono kwa jitihada zao.
"Hapa kuna wanafunzi 250 ambao shule hii isingekuwapo wangekuwa wanapata shida kutembea kila siku kwenda kule Chitare B na ukiangalia umri wao bado hawajaweza kuhimili mikikimikiki ya kutembea umbali mrefu kila siku,nitoe wito kwa wakazi wengine wa halmashauri yetu kuiga mfano huu" amesema kaimu afisa elimu huyo