Wanafunzi zaidi ya 40 wa shule ya Sekondari Kingalu, iliyopo Kata ya Kilakala, Manispaa ya Morogoro, wamenusurika kifo baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua kubwa iliyonyesha jana januari 25, 2023 wakati wakiendelea na masomo darasani.
Akizungumza juu ya tukio hilo Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Miyango Msilanga, amesema radi hiyo ilipiga kwenye madarasa ya kidato cha kwanza na cha tatu, na kusababisha madhara kwa wanafunzi zaidi ya 40 ambapo baadhi yao walipoteza fahamu, huku 25 wakilazimika kupelekwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Morogoro kwa matibabu zaidi.
Mkuu wa Shule hiyo, Miyango Msilanga amesema jumla ya wanafunzi hao 25 wa kidato cha kwanza na tatu ndio waliopata madhara makubwa na kufikishwa Hospitali.
Hata hivyo, Mwalimu Msiyanga amesema wanafunzi 17 kati ya 25 ndiyo wamebaki hospitali wakiendelea na matibabu.
Afisa Habari Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro Beatrice John amethibitisha kupokea Kwa majeruhi hao 25 (Wavulana 10 na Wasichana 15) na wanaendelea kupatiwa matibabu.
Akiongea akiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro mmoja wa majeruhi wa tukio hilo Salma omary (Mwanafunzi) amesema wakati wakiwa kwenye kipindi cha Hisabati mvua ilianza kunyesha kisha radi ikapiga kwenye swichi ya umeme ukutani.
“Ghafla nikaona mwanga mkali unatoka ukutani macho yakawa hayaoni hadi nafika Hospitali nilikuwa sioni lakini kwa sasa naona kidogo.”