Wanafunzi wawili wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Tumaini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia kwa kusombwa na maji wakati wakiogelea Mto Karanga.
Wanafunzi hao Lodrick Orota (14) na Ridhiwan Kimath (13) walifariki dunia Januari 27, mwaka huu wakati walipotoka shule na kwenda kuogelea mtoni.
Mwili wa Rodrick ulionekana jana Januari 30 baada ya kukaa kwenye maji kwa siku tatu, huku jitihada za kuutafuta mwili wa Ridhiwani zikiendelea kufanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema jitihada za kuutafuta mwili wa Ridhiwan zinaendelea baada ya jana kufanikiwa kuupata mwili wa Rodrick ambao walisombwa na maji tangu Januari 27.
Akizungumzia namna mwanaye alivyotoweka, baba mzazi wa Ridhiwan, amesema aliondoka nyumbani Januari 27 kwenda shuleni na ilipofika jioni mkewe alimweleza mtoto wake hajarudi nyumbani na ameanza jitihada za kumtafuta bila mafanikio.