Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi watoro kusakwa na mgambo

Wanafunzi Histori Wanafunzi watoro Njombe kusakwa na mgambo

Sat, 10 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Diwani wa Kata ya Kidugala iliyopo wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe, Wiston Mbilinyi ameagiza askari mgambo wa kata hiyo kuwasaka wanafunzi watoro shuleni na kuwapa adhabu ili warejee shule.

Agizo hilo amelitoa leo kwenye hafla ya kuwapongeza walimu wa shule za msingi zilizopo kwenye kata hiyo baada ya kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba uliofanyika mwaka huu nchini kote.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kupunguza utoro wa wanafunzi shuleni na kuongeza ufaulu ambao utasaidia kuinua kiwango cha elimu ndani ya kata hiyo.

Amesema mbali na watoto, hata wazazi wasiowafuatilia watoto wao kama wanafika shuleni, nao watasakwa.

"Mwenyekiti wa baraza la kata atahakikisha anasimamia haki, lengo letu siyo wananchi wafungwe bali kuwafanya wajue wajibu wao kwa watoto," amesema Mbilinyi.

Amewataka askari hao kutenda haki pindi wanapotekeleza majukumu yao ili yale yote ambayo yamekuwa kero ndani ya kata hiyo yaweze kutatuliwa.

Amewashukuru walimu wa shule katika kata hiyo kwa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu na kujitolea ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Ofisa elimu kata ya Kidugala, Felister Mgaya amesema jumla ya wanafunzi 153 walifanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu na wanafunzi 149 walifaulu mtihani huo.

Amesema pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto zinazochangia kurudisha nyuma maendeleo ya taalum ikiwemo upungufu wa walimu.

"Wazazi wengi wa madarasa ya mitihani huchangia kwa kuchanga fedha za uendeshaji wa mitihani ambayo wazazi kwa umoja wao wanakuwa wameridhia," amesema Mgaya.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kata ya Kidugala Alex Nyota amesema mafanikio hayo katika sekta ya elimu katika kata hiyo yametokana itekelezaji na usimamizi mzuri wa ilani ya chama hicho.

Chanzo: Mwananchi