Shinyanga. Wanafunzi zaidi ya 700 wa shule ya Sekondari Shinyanga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameandamana hadi ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwasilisha kilio cha manyanyaso wanayopata kutoka kwa walimu wao.
Baada ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 30 kuanzia saa 11 alfajiri leo Ijumaa Februari 14, 2020, wanafunzi hao wamekutana na kuwasilisha hoja zao kwa Mkuu wa mkoa huo, Zainab Tellack ambaye ameahidi kuzishughulikia.
“Ofisi yangu itayashughulikia malalamiko yenu. Nawataka kuwa watulivu wakati Serikali inafanya hayo na lazima muepuke kujiingiza kwenye migomo isiyo ya lazima inayoweza kuwapotezea muda wa masomo.”
“Lazima mzingatie tabia na maadili mema kwa kuacha vitendo vinavyoweza kukatisha ndoto zenu kielimu na kimaisha,” amesema.
Mkuu huyo wa Mkoa ameuagiza uongozi wa wilaya na halmashauri ya Kishapu kufika shuleni hapo kutatua changamoto za wanafunzi pamoja na maendeleo yao darasani.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, kaka mkuu wa shule hiyo, Mwendesha Manyangu ametaja miongoni mwa kero zao kuwa ni uongozi wa shule kutoshughulikia malalamiko ya adhabu zisizostahili zinazotolewa na baadhi ya walimu.
Pia Soma
- Majaliwa: Tusitumie corona kujipatia umaarufu
- Mbosso amlilia Boss Martha siku ya wapendanao
- Mafuriko yazoa daraja, wananchi wahaha kusaka huduma muhimu