Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi watakiwa kufichua wanaochoma shule

0821d6731ee908b0b64e928ad1bec9b5.png Wanafunzi watakiwa kufichua wanaochoma shule

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI katika shule za msingi na sekondari wameombwa kushirikiana na serikali kwa kuwafichua watu wanaohujumu na kuharibu miundombinu ya shule kwa namna mbalimbali ukiwemo ya uchomaji majengo ya mabweni na madarasa.

Kauli hiyo imetolewa juzi na wanafunzi wanaosoma shule za sekondari mkoani Dodoma walipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ibada maalumu ya wanafunzi kuiombea serikali. Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Mnadani Dodoma.

Akizungumza katika ibada hiyo, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya sekondari ya Dodoma, Michael Kusenah, alisema wao kama wanafunzi wakitoa ushirikiano wa dhati kwa serikali, upo uwezekano mkubwa kuwabaini haraka wanaohujumu na kuharibu miundombinu.

Alisema wanafunzi wana mchango mkubwa kuwezesha kubaini watu wanaoharibu miundombinu na hujuma nyingine hasa ikizingatiwa kuwa, wanaofanya hivyo wanaishi ndani ya jamii.

"Hivyo ninawaomba wanafunzi wenzangu kote nchini tutoe ushirikiano kwa serikali yetu tukufu kuhakikisha suala la uchomaji majengo ya shule linakomeshwa na hata wahusika wakibainika, mkondo wa sheria unachukua hatua kali," alisema.

Zacharia Mushi alisema uharibifu wa miundombinu unaofanyika katika majengo ya shule unarudisha nyuma maendeleo yao ya elimu, kwa kuwa muda mwingi wanafunzi wanakuwa katika hali ya mashaka na hofu ya kutokea majanga.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Watoto wa TAG, Jimbo la Dodoma Kati, Mchungaji Marcel Mushi, aliwataka wanafunzi kuendelea kuiombea serikali iweze kujenga shule na mabweni yanayohujumiwa kwa wakati.

Aidha, aliwaomba wanafunzi hao kutokatishwa na tamaa kutokana na hujuma hizo zinazofanywa kinachotakiwa kwa upande wao kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa serikali ili iweze kuwatambua na kuwachukulia hatua wanaobainika kuharibu miundombinu hiyo ya majengo.

Mbali na maombi hayo yaliyofanyika kwenye ibada hiyo mengine ni kuombea pia wanafunzi waliofaulu wapate vifaa vya shule kwa ajili ya masomo yao.

Chanzo: habarileo.co.tz