Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wataka taarifa za mwenzao aliyetekwa

35313 Pic+wanafunzi Wanafunzi wataka taarifa za mwenzao aliyetekwa

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Princes Gate, Mussa Idrissa amesema jana alikuwa na wakati mgumu baada ya wanafunzi wake kutaka kujua hatima ya mwenzao, Idrissa Ally aliyetekwa mwaka jana.

Idrissa (13), ambaye jana amefikisha siku 103 bila kuonekana, alitekwa Septemba 26, mwaka jana saa 11 jioni, alipokuwa akicheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti, Dar es Salaam.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST ambaye kabla ya kufanya kitendo hicho, alitoa kichupa kidogo na kumpulizia kisha kumuingiza katika mlango wa nyuma na kutokomea naye.

Akizungumza shuleni hapo jana, Mwalimu Mussa alisema wanafunzi hao ambao mwaka huu wameingia darasa la sita, walimfuata ofisini kwake wakati wa mapumziko ya saa nne asubuhi kutaka kupata taarifa za mwenzao.

“Baada ya kunisalimia wakaniuliza, vipi mwalimu rafiki yetu (Idrissa) ameshapatikana? Nikawajibu bado hajapatikana, lakini tusichoke kumuombea kila wakati. Hii ni mara ya pili wanafunzi hawa kuniuliza, mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana,” alisema.

Alisema jibu alilowapatia, lilionekana kutowafurahisha wanafunzi hao ambao aliwataja kuwa ni Aloyce Modest, Abdulswamad Sharif na Awatif Swaleh. Alisema walikaa kimya kwa dakika kadhaa na kumuuliza swali lingine, “Ina maana ndiyo hatarudi tena? nikawajibu bado anatafutwa, huenda akapatikana muda si mrefu ondoeni shaka.”

Wiki iliyopita, Leila Kombe mama mzazi wa Idrissa alisema, “Nashindwa nizungumzeje, miezi mitatu ni mingi sana, nimeshazoea sikukuu za mwisho wa mwaka tunakuwa wote nyumbani akinisaidia kazi mbalimbali. Bado nina uchungu na siamini kama mwaka mpya huu sikuweza kuwa na Idrissa.”

Leila, mama wa watoto wawili wa kiume, ambao ni Idrissa na mwenzake Ishack, aliwaomba Watanzania kumpa ushirikiano kwa kutoa taarifa polisi au kwenye vyombo vinavyohusika endapo watapata taarifa za mwanaye.

Kwa nyakati tofauti, Kamanda wa Polisi Kanda ya Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekuwa akinukuliwa akisema jeshi hilo halijapata taarifa zozote na upelelezi kuhusu suala hilo unaendelea.



Chanzo: mwananchi.co.tz