Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wasio na sare wilayani Kinondoni mwiko kurudishwa nyumbani

Wanafunzi wasio na sare wilayani Kinondoni mwiko kurudishwa nyumbani

Sat, 18 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wilaya ya Kinondoni imepiga marufuku wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka 2020 kurudishwa nyumbani kwa sababu ya kutokuwa na sare za shule.

Agizo hilo limetolewa jana Ijumaa Januari 17, 2020 na mkuu wa Wilaya hiyo, Daniel Chongolo katika hafla ya kuzipongeza shule na walimu waliofanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba mwaka 2019 kwenye wilaya hiyo.

Chongolo ametoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kuwa baadhi ya maeneo wanafunzi hawapokelewi kwa sababu ya kutokuwa na sare.

“Jambo la msingi kwa mwanafunzi ni kuripoti shule na kuwa na daftari na vifaa  vya kujifunzia, sijui hana sare, viatu au jembe, hicho si kigezo cha kutompokea.”

“Tumetoa ada ili kumfanya mwanafunzi mnyonge  kupata elimu basi tusiweke vigezo vitakavyoendelea kuweka mazingira ya kubaguliwa, wapokelewe wapewe elimu,” amesema Chongolo.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wazazi kujenga tabia  ya kujiandaa mapema, ikiwa ni pamoja na kuwaandalia watoto mahitaji yao ya msingi.

Akizungumzia sherehe ya utoaji tuzo kwa shule na walimu waliofanya vizuri, amesema wamefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kufika shule mapema na kuondoka jioni baada ya kutekeleza majukumu yao.

“Katika ufahamu wangu, ufaulu wa shule ndio utambulisho wa uzalendo na upendo wa walimu kwa nchi yao, walimu wana wajibu  wa  kuendelea kujituma zaidi kwa kuwa Tanzania ya kesho itaundwa na vijana  hawa walioko shuleni,” amesema Chongolo.

Awali, kaimu ofisa elimu wa manispaa hiyo, Chitegets Dominick amesema katika mtihani huo wa darasa la saba Kinondoni imeshika nafasi ya tatu kitaifa.

Chitegets amebainisha kuwa wanafunzi 12,523 walifanya mtihani wa darasa la saba katika wilaya hiyo, wavulana  waliofaulu ni 5,894 na wasichana 6,274.

Mwenyekiti wa walimu wakuu wa Wilaya hiyo, Odas Bambaza amesema katika matokeo hayo bado wanajiona ni wa kwanza kwa kuwa manispaa zilizoshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu, wote  wamepata asilimia 97 ila wamezidiana pointi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Meya wa manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta,  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Harlod Maruma.

Chanzo: mwananchi.co.tz