WANAFUNZI wasichana wapatao 220 kutoka shule 22 za sekondari wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro wamepatiwa elimu ya stadi za maisha , kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi , elimu ya kujitambua , kuepukana na vishawishi vitakavyowatumbukiza kupata mimba wakiwa wadogo.
Wanafunzi hao wamepatiwa elimu na mafunzo ya stadi za maisha kwenye kambi ya wasichana Kilosa iliyowekwa kuanzia Juni 21 hadi Juni 25, mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Dakawa , wilayani humo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema lengo la kuwakutanisha wanafunzi hao ni kuwapatiwa elimu ya stadi za maisha ikiwemo mbinu za kujikinga na virusi vya ukimwi , elimu ya kujitambua ili kuwaepusha na mimba za utotoni.
Profesa Kabudi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa alisema kambi hiyo itakuwa endelevu kila mwaka na kwa mwaka huu imefanyika kwa siku tano kuanzia Juni 21 hadi 25 mwaka huu.
Mkurugenzi Msaidizi, Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia ,Suzana Nyarumbamba akiwa kambini hapo alisema katika kipindi cha miaka mitano 2021 hadi 2026, serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari kwenye Kata ambazo hazina shule hizo zikiwemo 26 za wasichana na 717 za Kata.
Nyarumbamba alisema serikali ya awamu sita imedhamiria kuinua taaluma ya elimu hasa kwa watoto wa kike hivyo shule 26 za sekondari za bweni kwa wasichana zitajengwa kwenye kila Mkoa wa Tanzania Bara.
Mmoja wa wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Parakuyo , Rehama Kahaji kutoka jamii wa wafugaji wa Kimasai aliyeshiriki katika kambi hiyo alisema mafunzo hayo yamewasaidia hasa kutokana na jamii yao ya wafugaji kuwa nyuma na masuala ya elimu hasa kusomesha watoto wa kike .
Alisema changamoto kubwa inayowakabili wazazi hasa katika jamii ya wafugaji kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo na kuwaachisha shule kwa mtazamo wao kuwa mtoto wa kike hawezi kusoma bali ni wa kuolewa.
Hivyo alisema atatumia mafunzo na elimu aliyoipata kwenda kuwaelimusha wazazi na jamii ikiwemo ya wafugaji kuwa watambue wakiwasomesha watoto wa kike watakuwa wamejenga kizazi yenye maendeleo yao ya baadaye na Taifa.