Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wasababisha adha ya usafiri Ubungo

35226 Pic+ubungo Wanafunzi wasababisha adha ya usafiri Ubungo

Tue, 8 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Abiria katika kituo cha mabasi Ubungo wanaoelekea Tanga na Morogoro wamesema mabasi kukodishwa na baadhi ya shule kwa ajili ya kubebea wanafunzi ni sababu inayochangia uhaba wa usafiri.

Wametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 7, 2019 wakati wakizungumza na Mwananchi kuhusu hali ya usafiri ambayo tangu Januari 5, 2019 imekuwa si nzuri.

Hata hivyo, wamesema adha hiyo inaelekea kupungua, ingawa  abiria hulazimika kusubiri kwa muda mrefu badala ya kupata usafiri ndani ya muda mfupi kama ilivyozoeleka.

Samson Mafwimbo anayeelekea Morogoro amesema amefika kituoni tangu saa 1 asubuhi hadi anazungumza na gazeti hili saa 4 asubuhi hakuwa akiona dalili za kupata usafiri mapema.

“Hali hii inatokana na baadhi ya mabasi kukodishwa na wamiliki wa shule hasa msimu huu ambao wanafunzi wanafungua shule. Ila nimewauliza wahusika wameniambia kuwa nitapata usafiri lakini huenda ikawa jioni,” amesema Mafwimbo.

Amina Saleh aliyekuwa akielekea Tanga, amesema wamefika Ubungo saa 12 asubuhi lakini hawakupata mabasi badala yake wameelezwa kusubiri yanayotoka Tanga na wanatarajia kuondoka kuanzia mchana.

“Tumeshakata tiketi lakini tumeambiwa gari la kusubiria litoke Tanga. Hatuna jinsi maana muda huo wa mchana tungekuwa tumeshafika Tanga,” amesem Amina.

Kwa upande wake, Hamad Ally anayeelekea Morogoro ameungana na wenzake kwa kusema baadhi ya magari yamekodiwa kubeba wanafunzi wa shule mbalimbali wanaosoma mikoa kadhaa ikiwemo Morogoro.

“Nimekuja asubuhi na nimeshakata tiketi, lakini nimeambiwa gari litoke Morogoro ndiyo nitapanda kwa kweli tunapata shida sana hasa kwenye suala la muda,”amesema Ally.

Katibu mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu amekiri baadhi ya mabasi kukodishwa yakiwamo ya kampuni ya New Force kwa ajili ya kubeba wanafunzi.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Hassan Mchanjama amesema ni vyema mfumo wa usafirishaji ukabadilika ili kuondoa kero kwa abiria wanaosafiri wakati wa Januari.

“Magari mengi yamekodishwa, leo asubuhi zaidi ya mabasi saba ya kampuni ya New Force yamebeba wanafunzi kwenda mikoa mbalimbali ukiwamo wa Morogoro,” amesema.

Amesema ni wakati muafaka kwa wahusika kuangalia njia ambazo hazina abiria wengi wakati wa Januari baadhi ya mabasi yahamishiwe kwenye njia zenye changamoto kama  ya Morogoro na Tanga.



Chanzo: mwananchi.co.tz