WANAFUNZI 60 wa Shule ya Msingi Mloganzila A na B wenye uhitaji wamepewa msaada wa sure za shule na watumishi wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam baada ya kupokea sare hizo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mloganzila A, Jackson Massasi amewashukuru watumishi hao pamoja na uongozi wa hospitali ya Mloganzila kwa msaada huo na kuwaomba wawakumbuke tena wakati mwingine kwa sababu wanafunzi bado wana uhitaji.
“Mungu awabariki kwa msaada huu mliotoa kwa wanafunzi hawa, mmewagusa kwa kiasi kikubwa na siku zote wataendelea kuwakumbuka kila watakapokuwa wanavaa sare hizi,” amesema Massasi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dk Julieth Magandi amewapongeza watumishi hao kwa msaada waliotoa kwa wanafunzi hao ambao ni taifa la kesho.
“Matendo ya huruma ya namna hii ni kama ibada yenye baraka, hivyo matendo haya yasiishie kwenye kutoa sare za shule tu, nawaomba muendelee kujipanga kwa kadri mtakavyojaliwa ili kugusa jamii kwa upana zaidi,” amesema Dk Magandi.