Wanafunzi wanne wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa baada ya lori kugonga chumba cha darasa katika Shule ya Sekondari ya Kasaka iliyoko Halmashauri ya Mji wa Kanoni, Wilaya ya Gomba, nchini Uganda.
Kulingana na picha ambazo zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii kutoka nchini humo, lori hilo aina ya tipper linaonekana limepiga dafrau ukuta wa shule hiyo na kuubomoa kabisa pamoja na kuathiri sehemu ya paa la darasa hilo.
Polisi walisema kwamba tukio hilo lilijiri mwendo wa saa nane na nusu alasiri ya Jumatano wakati wanafunzi walikuwa darasani kwa mahudhurio ya masomo.
Wanafunzi watatu wa kati ya gredi ya 2 hadi ya 5 walifariki kwa majeraha kiasi huku wan ne akifariki baada ya kukanyagwa kiasi cha kutoweza kutambulika.
Atatambulishwa baada ya uchunguzi wa DNA kufanyiwa mabaki yaliyokusanywa kutoka eneo hilo la tukio.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Kefasi Katumba aliiambia Monitor kuwa dereva wa lori la Sinotruk aligonga lango la shule kwanza kabla ya kugonga maabara ya kompyuta na darasa la Senior Four West.
“Dereva anaonekana alishindwa kulidhibiti gari kwa kona na akafikiri lori litasimama iwapo atagonga lango la shule. Kwa bahati mbaya, liliendelea tu kusonga mbele kwa kasi, likaanguka kwenye maabara ya kompyuta ambapo liliua wanafunzi wawili papo hapo na kujeruhi wengine kadhaa.
"Lori hilohilo lilisonga mbele na kugonga darasa la Senior Four West ambapo pia liliua angalau mwanafunzi mmoja papo hapo na kuwajeruhi wengine,” alisema.
Zaidi ya hayo, wasimamizi wa shule walilazimika Jumanne jioni kuwarudisha wanafunzi wengine nyumbani hadi Jumatatu ijayo huku wakipata nafuu kutokana na mshtuko kufuatia mkasa huo.