Dodoma. Wanafunzi wanaopata mimba katika Shule ya Sekondari Kimagai wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma imepungua kutoka wanafunzi wanane mwaka jana hadi mmoja.
Hiyo ni baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) unaolenga wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Mradi huo unalenga kuwawezesha wasichana kupata elimu na mahitaji muhimu kama sare za shule, taulo za kike, vifaa vyote vya shule, chakula, kuwalipia nyumba kwa wanaotoka mbali ili kuwakinga dhidi ya maambukizi ya Ukimwi, mimba za utotoni na ngono zembe.
Akizungumza jana Jumatano Agosti 28, 2019 mkuu wa Shule hiyo, Veronica Mtiana amesema wasichana 22 wananufaika na mradi huo.
“Hadi hivi sasa Sh3.1milioni zimeshalipwa kwa ajili ya wanafunzi wanaonufaika na mradi huu. Kila mwanafunzi amepata Sh100,000 kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya shule zikiwemo taulo za kike nne kwa kila msichana,” amesema.
Amebainisha kuwa mradi huo umewezesha ufaulu kuongezeka, mwaka 2018 wanafunzi wanane walipata ufaulu wa daraja la pili ikilinganisha na mwaka 2017 ambako hakukuwa na mwanafunzi aliyefikia ufaulu huo.
Pia Soma
- 22 jela miezi sita kwa uzururaji, kujihusisha na biashara ya ngono
- Mikiki ya uchaguzi wa KKKT ilivyomrudisha Dk Shoo katika uongozi
- MAKALA YA MALOTO: Membe analo jambo la kumwambia Dk Slaa
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Winifrida Julius ameishukuru Serikali na Tacaids kwa kuwakumbuka wasichana waliopo katika mazingira hatarishi kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya shule.