Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wamduwaza DC na simulizi za unyago

49611 WANFNZ+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa wamemweleza mkuu wa wilaya, Hashim Mgandilwa kile wanachofundishwa kwenye mila za unyago.

Wanafunzi hao waliyasema hayo jana wakati wa baraza la wanafunzi na watoto wa kike wenye umri mdogo walio nje ya shule, lililoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Walimweleza Mgandilwa kuwa pamoja na kupewa mafunzo ya heshima, pia wanafundishwa kukata viuno ili baadaye wasiaibike kwenye ndoa.

Akizungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya, Grace Beatus, mkazi wa kijiji cha Kitandi aliyeacha shule alisema katika mila ya unyago wanafundishwa zaidi kukata viuno ili baadaye wasiaibike kwa waume zao.

“Hakuna vitu vya siri, kubwa kule ni kufundishwa jinsi ya kukata kiuno ili kiwe kilaini na tunafungiwa ndani kwa mwezi mmoja,” alisema Grace.

Alisema wakati mwingine wanafundishwa kukata viuno wakiwa wamefungwa vitambaa usoni.

Alisema wanapokuwa ndani wanavalishwa khanga au kaniki moja na hawaruhusiwi kuonana na watu wa nje.

“Wakati mwingine eneo tunalowekwa ndani ni karibu na barabarani, kwa hiyo tukiona watu tunajificha kwa sababu haturuhusiwi kuonana na watu.”

Msichana mwingine, Zainab Mnunduma aliyemaliza kidato cha nne, lakini akapata daraja sifuri alisema unyago una faida na hasara. “Una faida kwa sababu tunafundishwa heshima kwa wazazi. Kwa mfano tusiingie chumbani kwa baba na mama bila kugonga hodi na tuwaamkie asubuhi,” alisema.

Hata hivyo alisema sherehe za unyago zinachangia kudorora kwa uchumi akitoa mfano kuwa wakati msichana ‘anapotolewa ndani’ huandaliwa sherehe kubwa inayotumia fedha nyingi.

“Utakuta wanatumia hela nyingi kiasi kwamba sherehe ikiisha familia inaanza kupata shida na kulala na njaa,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mgandilwa alisema ili kuisaidia wilaya hiyo ni muhimu wananchi wakiwamo wanafunzi wakaangalia kama kweli mila ya ukataji viuno ina msaada kiuchumi.

“Hebu tuangalie faida na hasara za hivyo viuno mnavyofundishwa. Tupime faida zake na kama vina hasara, basi tuangalie uwiano,” alisema

Mgandilwa aliipongeza Tamwa kwa kuandaa baraza hilo ambalo limesaidia kuibua mambo mengi ambayo jamii au hata viongozi walikuwa hawayajui.

“Muendelee na kazi hii ya kukusanyika na wanafunzi wa kike na kuwapa elimu. Pia muwatumie hawa watoto wa kike walio nje ya shule wawe mabalozi wa kuhamasisha upingaji wa mila na desturi zinazoleta madhara.”

Alisema hakatazi mila za unyago, lakini ni vizuri zikafanyika wakati wa likizo ili zisiingiliane na masomo.

Pia alionya mitaala inayofundishwa katika unyago isiwe ya kuharibu maadili ya watoto wa kike.

Akizungumza katika baraza hilo, mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben alisema pamoja na mila na desturi elimu ni muhimu kwa watoto wa kike na shule zisitumike kama maeneo ya kukua tu, bali kupata ujuzi utakaowasaidia watoto hao na jamii zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz