Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi walivyomzawadia baiskeli mwalimu wao wa Hisabati

Mwalimu Baiskeli Wanafunzi walivyomzawadia baiskeli mwalimu wao wa Hisabati

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: Mwananchi

Ni hisia za furaha zilizopitiliza hadi kuleta machozi katika mashavu ya Emmanuel Kipaho ambaye ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Chamwino mkoani Dodoma baada ya kupewa zawadi ya baiskeli na wanafunzi wake.

Tukio hili linarandana na msemo unaosema ‘chanda chema huvikwa pete’, naam! hivi ndivyo unavyoweza kusema kwa jabali hili la somo la Hisabati ambalo hutembea takriban kilomita nane kila siku kuwahi kutimiza ndoto za watoto wa Kitanzania katika shule hiyo.

Kutokana na kujitoa kwa mwalimu huyo, wanafunzi wanaosoma kidato cha sita katika shule hiyo waliamua kumshtukiza kwa kumzawadia baiskeli.

“Kwangu ilikuwa ni surprise (kushtukiza) nilipigiwa simu na mwalimu mkuu msaidizi akinieleza kuwa wanafunzi wananihitaji shuleni Jumamosi (Julai 29, mwaka huu). Nikamuuliza kuna nini, hakunijibu badala yake akaniambia hafahamu,”amesema Kipaho.

Amesema siku hiyo aliamka asubuhi na kwenda zake mjini kwa ajili ya shughuli zake lakini ilipofika saa 6.00 mchana akapigiwa simu tena akiulizwa mbona hajafika, hali iliyomfanya kuona kuwa walikuwa na wanafunzi walikuwa na shida naye kweli na hivyo akaenda shuleni.

Amesema alipofika shuleni, wanafunzi hao walimtuma kiongozi wao wakimtaka aende darasani kwao, ndipo alipokwenda na alipofika walianza kumshukuru kwa kujitolea kuwafundisha baada ya muda wa kazi tena bila hata kuwadai malipo yoyote.

“Baada ya shukrani hizo wakaniambia tuelekee darasa la upande wa pili nikiwa na makamu mkuu wa shule, nilipofika hapo nikakutana na baiskeli waliyoninulia kwakweli nilijisikia furaha kwa jinsi walivyopokea kujitolea kwangu,”amesema.

Amesema zawadi hiyo inamfanya kuona ana deni la kulipa kwa wanafunzi hao kwa kuwawezesha kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kidato cha sita na hivyo kuinua ufaulu kwenye shule hiyo ambayo iko karibu na Ikulu ya Chamwino.

“Ushauri wangu kwa walimu wenzangu ni kuendelea kujitoa kwa ajili ya kuandaa Taifa letu. Sisi tunapita tu, tuhakikishe tunaacha kizazi kilicho bora ambacho kitaendeleza Taifa,”amesema.

Kipaho amewataka walimu wenzake kutoweka sana maslahi mbele yao mbele kwasababu kuna familia zina matatizo ya kiuchumi ambazo huhitaji walimu wawasaidie ili wafanikiwe.

Amesema pia wanapaswa kuelewa kuwa wao wapo walipo kwasababu kuna watu ambao walijitoa kwa ajili yao.

Kuhusu hofu ya kuwa hesabu ni ngumu, Kipaho amesema ni utamaduni tu uliojengeka kwa watu wengi lakini baada ya kuelewesha wanafunzi wanatambua somo hilo sio gumu.

Wanafunzi wazungumza

Mwanafunzi wa Kidato cha Sita, William Zawadi amesema wazo la kumpatia zawadi mwanafunzi huyo lilikuja baada ya kutambua kuwa wanafunzi wa shule nyingine hawakuwa wamefika mbali kama wao walipofika.

“Tulipokwenda likizo ya kumaliza kidato cha sita nyumbani, tukawauliza wenzetu wao wamefundishwa hadi wapi tukagundua kuwa sisi tuko mbali sana. Kwa kweli hili lilitugusa sana tukasema lazima tufanye kitu kwa mwalimu wetu angalau ajue tunadhamini mchango wake,”amesema.

Amesema mara baada ya kumaliza likizo, walipokuja walijadiliana na kuona kuwa wamnunulie baiskeli atakayoitumia kujia shuleni kwasababu hatuwezi kumnunulia gari.

Amesema katika fedha zao za matumizi kila mwanafunzi alijitolea Sh5, 000 na kufanya jumla ya Sh190, 000 wakaenda kumnunulia baiskeli.

Naye Cleopata Samwel amesema kumaliza mada (topic) mapema kutawawezesha kunafaidia kubwa kwao kwasababu kunawaweka katika nafasi nzuri ya maandalizi ya mitihani ya Taifa ya kidato cha sita.

“Muda huu hadi tutakapofanya mitihani mwakani tutautumia katika kufanya revision (marejeo) ya mitihani iliyopita na kuangalia wapo hatukuelewa vizuri tutamuuliza mwalimu atusaidie,”amesema.

Naye Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Oscar Machangu amesema mwalimu huyo ni mchapakazi na amekuwa akijitolea kwa kufika shuleni hapo saa 11.00 asubuhi na wakati mwingine jioni saa 12.00 hadi saa 3.00 usiku.

“Tunamtia moyo asichoke kujitolea kwa ajili ya wanafunzi hawa. Anabidii inayotokana na uamuzi wake mwenyewe bila kuambiwa na mtu afanye hivyo,”amesema.

Kuhusu nyumba, Machangu amesema kati ya nyumba 60 zinazohitajika kwa walimu wananyumba nne tu za walimu, jambo ambalo linawafanya wengi kusafiri umbali mrefu kila siku.

Kwa mujibu wa takwimu za elimu zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mwaka 2020, zinaonyesha mahitaji ya nyumba za walimu wa shule za sekondari ni 81,973, zilizopo ni 4,274 huku upungufu ukiwa ni 67,699.

Mbinu anazotumia

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi digital, Kipaho ambaye ni mwalimu wa Hisabati wa kidato cha tano na cha sita katika shule hiyo hutumia kati ya saa moja hadi mawili ya ziada kuwafundisha wanafunzi hao.

Amesema anatumia muda wa asubuhi kabla ya vipindi vingine vilivyo katika ratiba, kuwafundisha wanafunzi ama wakati mwingine jioni mara baada ya kumalizika muda wa masomo.

Amesema kwa kuwahi huko, kumemsaidia kubakiza mada moja ya Hisabati kati ya 18 anazotakiwa kufundisha kwa kidato cha tano na sita, 10 zikiwa za kidato cha tano na nane za kidato cha sita.

Amesema tangu alipowachukua kuwafundisha somo la hisabati kuna mafanikio makubwa wameyapata ambapo ufaulu umeongezeka mwaka kila mwaka.

Amesema matokeo ya kidato cha sita katika shule hiyo ya mwaka 2021, yanaonyesha ufaulu umeongezeka kwa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja F.

Amesema wanafunzi waliopata daraja daraja B walikuwa watano wakati waliopata daraja F wakiwa wawili na mwaka 2022 waliopata daraja A alikuwa mmoja huku F akiwa mmoja na ya mwaka 2023 daraja F lilikuwa ni moja na B walikuwa sita.

Amesema katika mwaka huu anategemea ufaulu kwa wanafunzi hao katika somo la hisabati utaongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa nyakati za nyuma kutokana na kumaliza topic mapema na ahadi za wanafunzi walizozitoa kwake.

Chanzo: Mwananchi