Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi walemewa na mabegi mazito

38757 Mabegi+%255Bpuic Wanafunzi walemewa na mabegi mazito

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miongoni mwa abiria waliokuwa wanasubiri usafiri katika kituo cha daladala Tabata- Matumbi, Dar es Salaam ni wanafunzi wanaosoma chekechea, madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari.

Kila mwanafunzi aliyeonekana kituoni hapo alikuwa amebeba begi lililohifadhi vifaa vya kujifunzia shuleni vikiwamo vitabu na madaftari.

Baadhi walionekana kubeba mabegi mazito zaidi kuliko umri na uwezo wao kuhimili mizigo hiyo.

Wakati wakiendelea kusubiri usafiri, mtoto mmoja wa miaka sita alilazimika kumuita dada yake akiomba kusaidiwa begi alilokuwa amebeba akilalamika kwamba ni zito.

“Dada! Nisaidie begi,” alisema mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa akivutwa na dada huyo kuelekea lililokuwa limesimama gari mbele kidogo ya walipokuwa, “Twende huko, usijidekeze.”

Japo majibu ya dada yalimnyong’onyeza, hakuwa na namna, aliendelea kubeba begi lake mpaka gari lilipokuwa.

Kwa nini wanabeba mabegi mazito kiasi hicho? Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa na waandishi wetu walisema hiyo ni kutokana na wingi wa masomo waliyonayo.

Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi St Marie, Hans Mwani alisema ameshazoea kubeba begi lake zito kwa sababu hufanya hivyo kila siku.

Baba yake, Orestas Mwani alisema hakuna shida kwa mtoto wake kubeba mzigo mzito kwa sababu kila siku huchukuliwa na gari kwenda shule na kurudishwa nyumbani.

“Sioni kama kuna tatizo kwa sababu kuna magari,” alisema mzazi huyo.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na chemba ya biashara nchini India mwaka jana umebainisha kuwa ubebaji wa mabegi mazito kwa watoto ni hatari na unaathiri misuli laini inayokua.

Lakini wakati utafiti huo ukibainisha hayo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya wazazi wanaamini kuwa watoto kubeba madaftari na vitabu vingi kila siku kunamaanisha kwamba shule husika inafundisha vizuri zaidi.

Asimulia mwanaye alivyoumia

Wataalamu wa afya na wadau wa elimu wanapinga ubebaji huo wa mabegi makubwa kwa wanafunzi wakisema ni hatari kiafya.

Kauli hiyo inathibitishwa na mkazi wa Tabata Kisukuru, Erick Mwamkinga akisema mwanaye alipata madhara makubwa kwenye bega lake la kushoto kutokana na kubeba begi zito.

“Aliumia bega lake la kushoto kwenye eneo la maungio ya begani na shingoni, eneo hilo liliachia kwa sababu begi lilikuwa zito zaidi,” alisema.

Mwamkinga alisema awali, walidhani kuwa mtoto wao ameumia kwa kuanguka au kujigonga na kitu wakati akicheza lakini baadaye wakagundua kuwa ni uzito wa begi.

“Tulipojua ikabidi tumpeleke hospitali alipopigwa picha ikaonekana bega lake lina shida. Bado anaendelea na matibabu,” alisema, “Unajua shule zetu hizi watoto wanabeba mizigo mikubwa ya madaftari kwa sababu walimu hawana vipindi maalumu na sisi wazazi hatujui. Ilibidi nianze kumsaidia kubeba daftari za siku hiyo tu.”

Alisema wakati mwingine wazazi hudhani ubora wa elimu unatokana na wingi wa mzigo kwenye begi la mtoto jambo ambalo sio sahihi.

Mbali ya Mwamkinga, mzazi mwingine, Ndekijile Kazembe alisema walimu katika baadhi ya shule huwalazimisha wanafunzi wanunue madaftari makubwa ‘counter books’.

“Fikiria namna hiyo madaftari yalivyo mazito halafu mtoto anabeba saba au 10,” alisema Ndekijile.

Alisema alimzuia mwanaye kubeba begi zito kwa sababu aliona anaelemewa.

“Nilimnunulia ile mifuko ya zamani inaitwa ‘sports’ hairuhusu madaftari mengi na nasimamia mwenyewe kuhakikisha habebi mzigo na anachukua madaftari ya masoko husika tu,” alisema Ndekijile.

Simulizi za wanafunzi

Wanafunzi wengi waliozungumza na Mwananchi walisema hawapendi kubeba mabegi mazito lakini wanalazimishwa kutokana na mazingira ya kujifunzia.

Wengi walisema wanashindwa kubeba madaftari kulingana na ratiba kwa sababu kuna wakati walimu huingia bila kuifuata hasa kipindi ambacho mwalimu mwingine haingii.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kunduchi, Abdallah Yahaya alisema kuna wakati huwa anahisi maumivu ya mgongo lakini hakujua kama begi lake zito linaweza kumsababishia madhara.

“Mwanzoni nilikuwa nachoka kutembea na begi lakini baadaye nikazoea na maumivu ya mgongo nayasikia zaidi kama nikicheza mpira,” alisema.

Mwanafunzi mwingine wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Msekwa, iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam aligundua kuwa anapata madhara kutokana na uzito wa begi lake akiwa darasa la nne.

“Darasa la nne ratiba ilikuwa haifuatwi lakini sasa hivi walimu wanafuata kwa hiyo nami niliacha kubeba madaftari mengi,” alisema.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Lusasaro, Prince Nyagawa alisema begi lake ni zito kwa sababu anapoanza mwaka huwa anabeba madaftari aliyokuwa anayatumia mwaka jana kwa ajili ya kujisomea.

“Humu kwenye begi kuna vitabu vya story, vya masomo, daftari za mwaka huu na nyingine za mwaka jana, ndio maana unaona zito, nimezoea kila siku huwa nabeba,” alisema Prince.

Mwanafunzi mwingine alisema kinachowalazimisha kubeba madaftari mengi ni hofu ya kuchapwa ikiwa mwalimu asiyekuwa wa somo husika ataingia.

“Wapo walimu ambao huwa wanafidia vipindi vyao, kwa hiyo unaweza ukashangaa ameingia darasani nawe huna kitabu wala daftari, wengine huwa wanatuchapa,” alisema mmoja wa wanafunzi na kuongeza;.

“Kuna siku kifua huwa kinauma sana kwa sababu ya begi, kila siku nabeba madaftari 15 ya masomo na ‘homework’ pia nabeba vitabu 12 ndio maana begi langu linaniumiza.”

Wanafunzi hao walisema wakati mwingine huwa inawawia vigumu kupanda daladala kwa sababu ya mabegi makubwa.

“Wakati mwingine abiria akituhurumia basi anapokea begi, na konda akiona tupo wengi anachagua wachache tu,” alisema Prince.

Kondakta wa daladala inayofanya safari zake kati ya Mbezi na Buguruni, Humphrey Kaisi alisema ukubwa wa mabegi ya wanafunzi hao wakati mwingine huwa unasababisha kero ndani ya daladala.

“Ukweli kuna makondakta huwa wanakataa wanafunzi sababu mojawapo ikiwa mabegi. Yanachukua nafasi kubwa, wanabeba mabegi mazito mno na wanaumia hawasemi tu,” alisema Kaisi.

Sababu za kubeba mabegi

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s-Tabata, Thomas Samson alisema fasheni ya kubeba mabegi ndiyo iliyosababisha wanafunzi wengi kujikuta wakibeba mizigo mizito kila siku wakati wa kwenda na kurudi shuleni.

Alisema wanafunzi wasiobeba mabegi mazito huonekana kama washamba kutokana na kuwapo kwa mtindo wa kisasa wa ubebaji mabegi ambalo alisema unahatarisha makuzi yao.

“Zamani sisi tulibeba mikoba kwa kushika mkononi, mabegi hayakuwapo na ukitaka kujua kwamba hii ni fasheni yanabebwa kuanzia chekechea hadi chuo kikuu,” alisema Samson na kuongeza;

“Shule yetu ina ratiba pia tunazo ‘diary’ (shajara) ambazo zina ratiba na kila siku mwalimu anajaza mwenendo wa mtoto, mzazi anaweza kumwekea mwanaye madaftari kulingana na masomo ya siku husika.”

Alisema kila shule ina ratiba na ingeweza kufuatwa kama kungekuwa na ushirikiano mzuri baina ya walimu, wazazi na wanafunzi wasingekuwa wanabeba mizigo hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Christ The King, Sister Mary Anastazia alisema wazazi wengi hawafuatilii masomo ya watoto wao hivyo hata kama kuna ratiba, wanafunzi hawawezi kujiongoza kuchagua madaftari ya kubeba kulingana na masomo.

“Mfano mtoto anaweza kuja na madaftari ya vipindi vya jana kwa sababu aliporudi nyumbani aliweka begi na asubuhi amechukua bila mzazi kulikagua. Mwalimu akiingia darasani anakutana na madaftari ya jana,” alisema Sister Mary.

Alisema shule yake ina ratiba ambayo imebandikwa kwenye ‘diary’ ya mtoto na kwa mzazi ambaye anafuatilia ni rahisi mwanaye kubeba madaftari ya masomo husika.

Utaratibu wa shule ya Msingi Anazak ya Dar es Salaam wa kuwaunganisha wazazi kwenye makundi ya ‘WhatsApp’ uliibua mjadala wa watoto kubeba mabegi mazito.

Mmoja wa wazazi hao, Tausi Adam alisema alipogundua kuwa mwanaye anayesoma darasa la tatu anabeba begi zito, aliibua hoja hiyo kupitia kundi lao.

“Mtoto wa darasa la tatu ni mdogo unakuta ana miaka saba au minane, sasa akibeba mzigo mkubwa unamuona kabisa anapata tabu mpaka kutembea,” alisema.

Alisema baada ya mjadala kwenye kundi lao, mwalimu wa darasa aliahidi kushughulikia jambo hilo.

“Siku chache akatupatia taarifa tayari watoto wanaacha madaftari na vitabu shuleni na nyumbani wanakuja na madaftari au vitabu vile tu vya masomo husika. Tunashukuru mwalimu wa darasa alitusikiliza,” alisema.

Mwalimu wa darasa la tatu katika shule hiyo, Ibrahim Sudi alisema utaratibu wa kuacha madaftari shuleni haufanywi kwa wanafunzi wa darasa la tatu pekee, isipokuwa la kwanza na la pili.

“Sio kwamba jambo hili halipo shuleni. Lipo lakini wazazi walitoa ushauri mwanzoni kabisa ya mwaka wakati bado kuna harakati za kufungua shule,” alisema.

Mwalimu mwingine wa darasa la pili, Henry Godfrey alisema wanafunzi katika darasa lake wanaacha madaftari shuleni na kurudi nyumbani na vitabu.

Wadau wa elimu

Mtaribu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Cathleen Sekwao alisema anatamani ianzishwe kampeni ya kumtua mtoto begi mgongoni ili kuhamasisha shule zisimamie ubebaji kulingana na masomo ya siku husika.

Semkwao alisema wapo baadhi ya walimu wanaosababisha watoto kubeba madaftari na vitabu vya masomo yote kutokana na mtindo wao wa kuingia darasani bila kufuata ratiba.

“Jambo hili linawaathiri watoto kwa kiasi kikubwa japo jamii ipo kimya kama haielewi. Athari za ubebaji huu hazionekani haraka na zinachukua muda mrefu,” alisema Sekwao.

Alisema lazima uandaliwe mkakati utakaowasaidia watoto kutobeba vitu vingi kwenye mabegi yao ili kunusuru afya zao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoa Elimu Wasiotegemea Serikali, Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamin Mkonya alisema jukumu la kuwapunguzia mzigo wa madaftari na vitabu wanafunzi lipo ndani ya utawala wa shule.

“Kinachopaswa ni kuwekewa kanuni kuwa kila mwanafunzi asije na mzigo unaozidi gramu 500 na hilo litafanikiwa ikiwa ratiba za vipindi shuleni zitaheshimiwa na walimu,” alisema.

Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Azanak, Joseph Marwa alishauri kuwapo kwa sera itakayoelekeza namna wanafunzi wanavyoweza kutua mizigo ya mabegi makubwa.

Alisema, sera hiyo lazima pia ipunguze idadi ya masomo kwa wanafunzi hasa wa madarasa ya chini ambao mara nyingi wanakuwa hawajakomaa.

“Suala la mabegi kwa watoto tuliliona muda mrefu, ikabidi kila darasa tutujenge makabati kwa ajili ya kuhifadhia madaftari na vitabu, utekelezaji wake ndio changamoto,” alisema Marwa .

Alisema changamoto inayowakabili katika utekelezaji ni baadhi ya wazazi kutaka watoto wao waende na kurudi na vitabu kila siku hivyo kuwabebesha wanafunzi mzigo.

Mwalimu na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Neema Mponela alisema mwanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la tatu hapaswi kubeba vitabu ya masomo yote yanayofundishwa.

“Wakati mwingine begi kubwa linaweza kuondoa usikivu wa mtoto kwa sababu hata mwalimu akiingia atatumia muda mrefu kutafuta daftari, akiliona akili yake inakuwa tayari imeshahama na mwalimu ameshaanza kufundisha,” alisema.

“Watoto wetu wanatakiwa wasaidiwe kwa sababu wanateseka japo jamii ipo kimya haijui kama anateseka,” alisema.

Kauli ya Serikali

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alisema ingawa wizara haijatoa mwongozo wa aina ya mabegi yanayopaswa kubebwa na wanafunzi, si busara kumbebesha begi zito mtoto mdogo.

Alisema hata Sheria ya Mtoto inazuia kumtumikisha kama kumbebesha mizigo mzito.

“Hata kama bado hatujatoa vigezo vya mabegi, lakini mwalimu au mzazi usimbebeshe begi kubwa mtoto,” alisema.

Alisema ingawa hawajapokea malalamiko, lakini kunahitajika kukaa na kutoa mwongozo wa namna ya mabegi kwa wanafunzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz