Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wa kwanza, pili kitaifa waeleza siri ya ufaulu

38337 Mwanafunzi+pic Wanafunzi wa kwanza, pili kitaifa waeleza siri ya ufaulu

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Hope Mwaibanje, aliyeshika namba moja kitaifa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018 na mwenzake, Avith Kibani ambaye amekuwa wa pili wameeleza siri ya kufanya vyema, licha ya changamoto nyingi walizozipitia.

Wakati Kibani akisema ndoto yake ni kuwa daktari wa magonjwa ya moyo, Mwaibanje alisimulia jinsi alivyokuwa akilazimika kutumia kibatari kujisomea kutokana na nyumba wanayoishi kutokuwa na umeme.

Jana, Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), lilitangaza matokeo hayo, huku Mwaibanje aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari Ilboru mkoani Arusha na Kibani wa Marian Boys wakishika namba moja na mbili.

Mwaibanje, mtoto wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto sita alisema, “makazi yetu ni ya kawaida kama unavyoyaona (huku akionyesha mandhari ya nyumba). Tunaishi nyumba haina umeme na mimi nilipokuwa nikija likizo nilikuwa natumia kibatari kujisomea.”

“Niliona ni hali ya kawaida kwangu na nashukuru Mungu nimefanya vizuri katika matokeo yangu.”

Alisema kujituma katika masomo kulitokana na ushauri aliokuwa akipewa na mama yake, Ikupa Cosmas aliyemtaka asome zaidi ili aikomboe familia yao.

“Shuleni kulikuwa na ushindani mkubwa katika masomo na mimi nilitokea shule za mtaani, ila nilijituma kutimiza nia yangu ya kuwa daktari bingwa wa moyo. Nikianza kidato cha tano nitasoma Fizikia, Kemia na Baiolojia,” alisema Mwaibanje akifichua pia kuwa darasa la saba alishika nafasi ya tano kimkoa.

Kaka wa Mwaibanje aitwaye Nicholas alisema mdogo wake anapenda kucheza mpira, lakini alikuwa hasahau ratiba yake ya masomo.

“Kaka yetu ana shahada ya elimu, mimi (Nicholous) nina shahada ya usanifu majengo, lakini kwa bahati mbaya wote hatujapata ajira. Sasa hivi tumejikita kwenye ujasiriamali, wadogo zetu wawili wameishia kidato cha nne na wa mwisho yupo darasa la nne,” alisema.

Kwa upande wake, Kibani anayeishi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera alieleza jinsi anavyopenda kupiga kinanda akiwa shuleni, nyumbani na kanisani, huku akiwa na ndoto ya kuwa daktari.

“Nataka kuwa mtaalamu wa matatizo ya moyo kwa sababu nchi nyingi za Afrika naona hatujawa na wataalamu wa kutosha katika eneo hilo, watu wanaingia gharama kubwa kutafuta matibabu nje ya nchi. Natamani huduma hiyo ipatikane kwa wingi hapa nchini,’’ alisema Kibani.

Mwanafunzi huyo ambaye alikuwa kiranja wa afya na mazingira shuleni, alisema kinachozitofautisha shule binafsi na zile za Serikali katika ufaulu ni usimamizi mkubwa wa nidhamu uliopo sambamba na miundombinu rafiki inayowapa fursa wanafunzi kujifunza.

Kabla ya kujiunga na Marian Boys, Kibani alisoma katika Shule ya Kibeta English Medium iliyopo Manispaa ya Bukoba na katika matokeo ya kidato cha pili alishika nafasi ya tano kitaifa upande wa wavulana.

>>Matokeo kidato cha nne 2018 haya hapa

Marian Boys wafunguka

Makamu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Marian Boys iliyoshika nafasi ya tatu kitaifa, Gesase Mlimi alisema kujidhatiti kwa walimu na wanafunzi kwenye masomo ni sababu mojawapo iliyochangia kufanya vizuri mitihani ya kidato cha nne

Mbali na shule hiyo kuingia katika orodha hiyo, pia imetoa wanafunzi wanne walioingia kwenye kundi la kumi bora waliofanya vizuri kitaifa.

Tanga washtushwa

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi mkoani Tanga walionyesha kushtushwa na matokeo hayo kutokana na shule tatu kati ya 10 zilizofanya vibaya kutokea mkoani humo. Shule hizo ni Kwediboma, Komkalakala na Seuta.

Mzazi wa wanafunzi wawili wanaosoma Shule ya Sekondari Seuta, Sufiani Daudi alisema anashangazwa na shule hiyo kushika mkia wakati ipo mjini.

“Ipo mjini Songe ambako ni makao makuu ya wilaya (ya Kilindi) na wanafunzi hawana changamoto ya usafiri na kila huduma zinapatikana. Imenishangaza,” alisema Daudi.

Diwani wa Kata ya Kwediboma zilipo shule mbili kati ya tatu zilizoshika nafasi za mwisho mkoani humo, Mwajuma Sempule, alisema hawakutarajia matokeo hayo, huku mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mussa Semdoe akisema waliweka mikakati ya kupandisha ufaulu, lakini hali imekuwa tofauti.

Zanzibar kama Tanga

Kama ilivyo Tanga, shule nyingine tatu zilizofanya vibaya zipo visiwani Zanzibar ambazo ni Kijini na Pwani Mchangani (zote Kaskazini Unguja) na Ukutini iliyopo Kusini Pemba.

Wakizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baadhi ya walimu wa shule hizo walisema sababu ya kutofanya vizuri zimechangiwa na mambo mbalimbali ikiwamo ushirikiano mdogo kati ya walimu na wazazi, uhaba wa walimu pamoja na utoro wa wanafunzi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ukutini, Rashid Mohamed alisema uhaba wa walimu umechangia kufanya vibaya katika mitihani hiyo.

Alisema badala ya kuwa na walimu 13 wapo tisa wanaofundisha wanafunzi wengi.Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini ‘A’ Unguja, Riyami Haji Bakar alisema jambo kubwa linalochangia kufanya vibaya katika mitihani yao ni utoro uliokithiri wa wanafunzi.

Alisema katika darasa lenye wanafunzi zaidi ya 60, wanaohudhuria wanaweza kuwa 30 au chini ya hapo.

Riyami alisema wazazi na walezi wanatambua suala hilo, lakini hawachukui hatua za kuwasaidia walimu.

Alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika lakini kutokana na wazazi na walezi kuwa kitu kimoja na watoto wao inakuwa vigumu kwa walimu kufikia malengo waliyokusudia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kijini Mkoa wa Kaskazini ‘A’ Unguja, Ulimwengu Mkadam Makame alisema ushirikiano mdogo kati ya walimu na wazazi umechangia wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani hiyo.

Alisema wamekuwa wakiandaa mikakati mingi ambayo inahitaji kuungwa mkono na wazazi, lakini wazazi wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano.

Kwa habari zaidi kuhusu matokeo ya kidato cha nne tembelea mtandao tovuti yetu:

www.mwananchi.co.tz

Imeandikwa na Phinias Bashaya (Bukoba), Ipyana Samson (Mbeya), Burhani Yakub (Tanga), Bakari Kiango (Dar) na Haji Mtumwa (Zanzibar)



Chanzo: mwananchi.co.tz