Halmashauri ya Jiji la Tanga kupitia mradi wake wa ‘Inspire’ imepanga kuongeza hamasa ya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi ili kuzalisha wataalamu na wabunifu wengi zaidi.
Hayo yalisemwa na Ofisa Elimu Taaluma Sekondari jijini hapa, Daudi Nchia wakati wa ufunguzi wa kongamano la sita la sayansi kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari nchini.
Alisema kupitia mradi huo wanafunzi wanaweza kupata fursa ya kufanya majaribio ya kisayansi kupitia kituo cha sayansi ambapo watajifunza majaribio ya kisayansi na kuwawezesha kubuni vifaa na mbinu mpya za kiteknolojia.
“Nchi yetu inapungukiwa na wataalamu wa sayansi kulingana na uhitaji wa sokoni uliopo, hivyo katika kukabiliana na uhitaji huo jiji tumeanza mikakati ya kuwahusisha vijana wa shule za msingi na sekondari katika kuwa wabunifu kwenye sekta hii,” alisema Nchia.
Alisema malengo yao ndani ya kipindi cha miaka
mitano na 10 wakati taifa likiwa limekwenda mbali katika masuala ya teknolojia, mafanikio ya kuwapo kituo cha sayansi mkoani Tanga yatakuwa yameanza kuonekana kwani vijana wengi watakuwa wamekuwa wabunifu.
Meneja wa Kituo cha Sayansi cha Stemp Park, Gipson Kawago alisema kongamano hilo limejumuisha wanafunzi 70 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari nchini.
Alisema katika kituo hicho wanafunzi watajifunza majaribio mbalimbali ya kisayansi na teknolojia kwa vitendo ambayo wakati wakiwa shule walikosa nyezo na vifaa vya kufanya mazoezi hayo na hivyo kuishia kujifunza kwa nadharia pekee.
“Wataweza kujifunza namna ya kurahisisha utoaji wa huduma katika vituo vya afya kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki kwa kusafirisha vifaa tiba na dawa kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” alisema Kawago.
Naye Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga, Dk Charles Mkombe alisema matokeo ya majaribio hayo watayatumia kuboresha huduma zao kwenye vituo vya afya, hivyo wananchi wataweza kupata huduma bora na kwa haraka zaidi.
“Kwa kutumia ‘app’ ambazo zitakuwa katika simu janja, mtaalamu wa afya ataweza kuwasiliana na mtaalamu mwenzie aliyeko kwenye kituo kingine na kubadilishana taarifa au kushauriana kitaaluma kuhusu changamoto zilizopo za huduma na namna ya kupata ufumbuzi,” alisema.
Wanafunzi walioshiriki kongamano hilo walisema limewasaidia kuwa wabunifu na hivyo kuwaongezea hamasa ya kupenda masomo ya sayansi kutokana na kupata fursa ya kubadilishana mawazo na wenzao pamoja na kujifunza vitu vipya.
“Niwaombe wazazi pindi ambapo fursa kama hizi zinatokea wawashirikishe vijana wao kwani huku wanaweza kujifunza vitu vingi na hivyo kuwa wabunifu,” alisema Innocent Simon.
Naye, Nabiha Ally alisema kupitia kongamano hilo amejikuta anapenda somo la hesabu ambalo hapo awali alikata tamaa kutokana na kuona ni miongoni mwa masomo magumu lakini sasa amejifunza mbinu rahisi za kuelewa somo hilo.