Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi Rombo kula samaki mashuleni

Samaki Mafuta Mafuta Wanafunzi Rombo kula samaki mashuleni

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imetenga zaidi ya Sh128 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bwawa la samaki katika kijiji cha Momwe, Kata ya Mrao Keryo, wilayani Rombo ambapo kukamilika kwa mradi huo kutawezesha wanafunzi kupata kitoweo hicho katika milo yao mashuleni.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara, Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ambaye aliongozana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde amesema mradi huo utakapokamilika utatumika kama shamba darasa katika wilaya hiyo ili kuongeza uzalishaji wa samaki na kunufaisha wananchi wa wilaya hiyo.

"Faida ya huu mradi ni nyingi sana, tunataka watu wale vizuri, wale samaki, kweli tunakula nyama ya mbuzi, ng'ombe lakini tunahitaji samaki na kadri tunavyozalisha samaki wengi na shule zetu watoto wataanza kula vizuri," alisema Profesa Mkenda

Amesema eneo hilo ambalo lina ukubwa wa zaidi ya ekari mbili litazalisha samaki wa kutosha na kusaidia kulisha shule za kata hiyo pamoja na kata jirani za wilaya hiyo na kwamba utasaidia kuongezea kipato kwa mwananchi mmoja mmoja.

"Eneo hili ni kubwa na huu mradi utakapokamilika tutapata samaki wengi wa kutosha, tunataka mradi huu utakapoanza halmashauri itenge fedha kidogo na sisi serikali tutachangia, tunataka tuone watoto wetu wakienda shuleni wanakula,"

Profesa Mkenda aliishukuru serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia, Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Naye, Naibu Waziri Silinde amesema mradi huo utakapokamilika utatumika kama shamba darasa katika wilaya hiyo na kwamba tayari mchakato wa upatikanaji wa fedha hizo uko mahali pazuri kwa ajili ya kuanza ujenzi huo mwaka huu.

"Wizara tumeshaandikia Hazina kuomba fedha kwa ajili ya mradi huu wa hapa Momwe na katika hatua za awali mradi huu utagharimu sh128 milioni, lengo ni wananchi wa eneo hili kunufaika na mradi huu,"

Silinde, amempongeza Profesa Mkenda kwa namna ambavyo amekuwa akipigania miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo na kusema kwa kipindi cha miaka miwili katika wilaya hiyo amefanya mambo makubwa.

"Tuhakikishe huu mradi tunausimamia na tunaulinda vizuri, maana serikali inapambana kuhakikisha inaleta maendeleo katika maeneo haya ya wananchi ili muweze kunufaika na miradi hii ambayo inatekelezwa na serikali yetu,"

Anisia Tesha na Amani Joseph, wakazi wa Kijiji cha Momwe, walisema mradi huo utakapokamilika utasaidia wananchi wengi kupata fursa ya kujishughulisha na biashara ya samaki katika wilaya hiyo na kuongeza kipato cha familia na kwamba itasaidia kubadilisha mlo wa mara kwa mara badala ya kula nyama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live