Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi Longido wapewa taulo za kike 400

11145 Pedi+pic TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha.Mbunge wa jimbo la Longido mkoani Arusha, Steven Kiruswa  na mkewe Agnes Kiruswa na rafiki yao raia wa Marekani Sarah Messenger wamegawa taulo za kike 400 zinazoweza kutumika na kufuliwa tena kwa wanafunzi wa shule nane za Msingi na Sekondari wilayani Longido.

Akizungumza leo Julai 10 katika hafla ya kukabidhi taulo hizo, Dk Kiruswa alisema msaada huo utasaidia kuwaondoa wanafunzi hao katika adha ya kukosa masomo wakati wa siku zao za hedhi .

Dk Kiruswa alisema msaada huo pia umekuja wakati muafaka kwa jamii hiyo ya kimasai ambayo ina uhitaji mkubwa kutokana na kuwa na kipato cha chini kumudu gharama za taulo hizo kila mwezi.

"Julai Mosi mwaka huu Bunge pia lilipitisha azimio la taulo hizo kuondolewa kodi na Serikali kukubali na tayari kodi hiyo imeshaondolewa,’’ alisema.

Kwa upande wake Messenger alisema yeye na kinamama wenzake wa jimbo la Michigan walikubaliana na kuanza kufanya harambee katika maeneo mbalimbali ikiwamo shuleni na kanisani na kupata fedha ambazo walinunua zana za kutengenezea.

"Tulianza utaratibu wa kukutana kila Jumatano jioni na kufanya kazi ya kushona taulo hizo katika vikundi vyetu mbalimbali," alisema.

Alisema kiasi hicho cha taulo zilizotolewa ni kama kwa majaribio lakini iwapo zitaonyesha ufanisi na kuwafaa watoto hao wataletewa nyingine hadi pale itakapoonekana mahitaji yamejitosheleza na kuwa na ziada za kutosha kwa wanafunzi wa shule zote wilayani humo.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mhina alisema msaada huo una maana kubwa na taulo hizo ndizo zinazofaa kulingana na mazingira ya Longido.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz