Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 800 wafundwa afya ya akili

Wanafunzi 800 Wanafunzi 800 wafundwa afya ya akili

Tue, 18 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Zaidi ya wanafunzi 800 wenye mahitaji maalumu kutoka Shule ya Sekondari Kazima iliyopo mkoani Tabora wamepewa mafunzo ya kukabiliana na matatizo ya afya ya akili na namna ya kukuza kipato cha muda mfupi kupitia kilimo cha mboga mboga.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na Shirika la Akili Platform Tanzania yaliwajumuisha pia wazazi wenye watoto wenye ulemavu ambao wamefundishwa kilimo mviringo (kilimo cha kupanda kwenye mifuko) ili kujikwamua kiuchumi na kuweza kulea watoto wao.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Roghat Robert amesema wametoa elimu hiyo ili kuwajengea uwezo wanafunzi kushinda hofu, wasiwasi, msongo wa mawazo na namna ya kuongeza kipato kupitia kilimo cha mboga pindi watakapohitimu masomo yao.

“Tumepanda miche ya Karoti, Beetroots, Chinese na viazi lishe ili kuendana na kauli mbiu ya Serikali inayohamasisha lishe shuleni, tuna amini hayo mazao ambayo tumepanda yakitunzwa kwa uaminifu mkubwa wanafunzi wataanza kula mboga kupitia mikono yao kwahiyo itasaidia kupunguza zile gharama zilizotakiwa kununua vitu hivyo na badala yake watatumia fedha hizo katika matumizi mengine shuleni hapo,”

“Nitoe wito kwa wakuu wa shule za msingi, sekondari na vyuoni kuendelea kuitumia shirika hili kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu masomo yao wawe na uwezo wa kujitegemea kupitia kazi za mikono yao,”amesema Roghat

Mbali na elimu hiyo kwa wanafunzi, amesema wamewafunda wakazi wa mkoa huo kuhusu kilimo cha mviringo kinachotumia mifuko na kuwagawia mbegu za mboga mboga na viazi lishe lengo likiwa kila kaya kuwa na uwezo wa kumiliki mifuko 500 ya mazao hayo.

“Nitoe wito kwa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kuwekeza katika kilimo cha mboga mboga ambacho kitawasaidia kuwapa matokeo ndani ya muda mfupi hivyo kuwasaidia kuwalea watoto wao katika afya na malezi bora,” amesema Roghat

Mwalimu wa Mazingira Shule ya Sekondari Kazima, Clemence Mwamasega ametoa wito kwa uongozi wa shirika hilo kuongeza idadi ya mbegu za viazi lishe shuleni hapo ili kuokoa gharama kubwa ambayo wamekuwa wakiitumia kununua vitafuno.

Nao wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru elimu hyo wakisema wataitumia kwa vitendo ili kujiongezea vipato pindi watakapohitimu masomo yao.

Chanzo: Mwananchi