Wanafunzi 800 kati ya 86,000 wanaosoma shule za msingi 86 zilizopo Kasulu mkoani Kigoma wameshindwa kuendelea na masomo baada ya wazazi kuwahusisha na shughuli za kilimo.
Afisa elimu wilayani humo, Joseph Maiga, ameyabainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema hali hiyo ya utoro inatokana na kuanza kwa msimu wa kilimo ulioanza Septemba na amabo utamalizika Machi 2021
Katika msimu wa kilimo mara nyingi watu hufanya shughuli za kilimo vijijini, huku wakiwatumikisha wanafunzi.
Amesema moja ya sababu ambayo huwafanya watoto hao kushindwa kuendelea na masomo ni wazazi kuwashirikisha watoto katika malezi na hivyo kuwalazimu wanafunzi hao kubaki nyumbani ili kuchukua jukumu la kulinda nyumba na kuwahudumia watoto wadogo wasioweza kujihudumia.
“Sambamba na hilo katika mwaka 2020-2021, tumeweza kubaini mimba kwa watoto 2, inaumiza kuona namna gani wazazi wanaharibu kwa makusudi ndoto na maisha ya watoto wao na ni ukatili mkubwa mno,” amesema Maiga.
Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Kasulu, Pelimina Msuta, amesema suala la wazazi kuwaacha watoto kwa ajili ya kilimo ni jambo la kawaida na kwamba badala ya kwenda shule huamkia kutafuta vibarua ili wapate kipato cha kuwalisha wadogo zao na wengine hushinda sokoni wakiomba chakula.
Amesema inasikitisha kuona jamii inashindwa kuelewa umuhimu wa elimu kwa watoto na kushindwa kujipanga wao kama wazazi kuwalea watoto na kusababisha utoro wa makusudi na mbaya zaidi wazazi wanaandaa kuharibu kizazi kijacho.
Akiongea kwa niaba ya wazazi Magdalena Pius mkazi wa kijiji cha Nyakitonto amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa suala la malezi ya aina hiyo linasababishwa na umaskini uliopo ngazi ya familia na hivyo mzazi kuamua kusaidiana na watoto wake kufanya malezi, hasa kwa familia ambazo zinasimamiwa na mzazi mmoja kimapato.