Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 68 Maswa wapata mimba

Cd868f5f1a07dae958f5cadfc45f1f86 Wanafunzi 68 Maswa wapata mimba

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMLA ya wanafunzi 68 kutoka shule za msingi na Sekondari katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamepata ujauzito katika kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba mwaka huu.

Taarifa ya Jeshi la Polisi wilayani humo dawati la jinsia, imeeleza kuwa shule za msingi ni wanafunzi watatu wakati wa sekondari wakiwa wanafunzi 65.

Idadi hiyo imetajwa na mkuu wa dawati hilo, Anande Masai wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupiga vita ukatili wa kijinsia wilayani humo yaliyofanyika kijiji cha Shishiyu na kuratibiwa na Shirika la Worldvison Tanzania.

Anande alisema kuwa jumla ya kesi 27 zilihusisha mimba za wanafunzi hao na ndio zilifikishwa mahakamani na nane kati ya hizo zimetolewa hukumu, 10 zinaendelea kusikilizwa na sita zimeondolewa mahakamani.

Alieleza kuwa jamii bado imeendelea kuficha taarifa za matukio hayo ya mimba kwa wanafunzi kwa kumalizana kienyeji, ikiwa pamoja na kushindwa kutoa ushahidi mahakamani kwa baadhi ya kesi ambazo zipo katika chombo hicho cha haki.

Mbali na mimba Anande alisema kuwa katika dawati hilo wamepokea matukio 148 ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na matukio 195 kwa watu wazima wakiwemo wanaume 20 kwenye wilaya hiyo.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mratibu wa Worldvison Tanzania Mradi wa maendeleo ya jamii Shishiyu, Yohana Masanja aliwataka wadau wote kuungana kwa pamoja kuhakikisha vitendo hivyo vya ukatili vinakomeshwa kwenye jamii.

Aidha Masanja alisema kuwa elimu endelevu kwa jamii inatakiwa kila wakati ili kuhakikisha inatambua haki ya kila mtu, ikiwa ni pamoja na kuondokana na mitazamo hasi, imani au desturi ambazo zimepitwa na wakati.

Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo Fredrick Lukuna aliwataka wazazi na walezi kuacha kukwepa majukumu yao kulea watoto.

“Siku hizi wazazi na walezi wamewaachia walimu kulea watoto wao, hawataki kubeba majukumu yao kama wazazi, wamewaachia watu wengine ambao ndiyo wamekuwa wakiwafanyia vitendo hivi watoto na kuwapa mimba," alisema Lukuna.

Chanzo: habarileo.co.tz