Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 600 waliokosa malezi bora wawezeshwa

Sat, 27 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Shirika la SOS Children’s Villages Tanzania limewatambua na kuwawezesha wanafunzi 600 wa shule nane za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Wanafunzi hao ni wale  waliokosa  malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi wao.

Mwakilishi wa shirika hilo, Francis Mwakinga ametoa taarifa hiyo leo kwenye tamasha la ulinzi na usalama wa mtoto lililofanyika katika uwanja wa Luang’a kata ya Kising’a mkoani Iringa.

Alizitaja shule wanazotoka wanafunzi hao ni  Hoho, Mawindi, Chamdindi na Ikengeza kwa upande wa kata ya Nyang’oro na Iguruba, Makadupa na Isaka kwa kata ya Malengamakali na Ulanda na Chamdindi kutoka kata ya Ulanda.

Alisema mbali na mafunzo wanafunzi hao wamepewa vifaa vya kujifunzia, sare za shule, viatu na mabegi.

Mwakinga alisema kabla ya kuwafikia wanafunzi hao na kuwapa misaada hiyo walikuwa wanajihisi tofauti na watoto wengine kwa sababu walikosa mahitaji mengi waliyonayo wanafunzi wenzao hivyo walikata tamaa na shule na baadhi yao walikuwa watoro na hawakuwa na furaha wawapo shuleni.

Alisema msaada huo umetolewa kupitia mradi wao ulioanza kutekelezwa mwaka 2017 wilayani humo ukilenga kuboresha mazingira ya elimu, ulinzi na usalama wa mtoto na kuhakikisha jamii na Serikali inaipa kipaumbele haki ya elimu kwa mtoto na inaweka bajeti rafiki kwa kundi hilo.

“Lengo kuu la shirika kutetea haki za watoto walio katika hatari ya kupoteza malezi na kwa wilaya ya Iringa tumepanga kuwafikia wanafunzi 1,200 hadi mradi huu wa miaka mitatu utakapokamilika,” alisema na kutaja mikoa mingine inayonufaika na mradi huo kuwa ni Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Seleman Pandawe alisema katika tamasha hilo lililoshirikisha wanafunzi wa shule hizo, walimu, walezi na wazazi, kwamba watoto wengi wamekuwa wakipoteza haki zao za msingi kwa sababu ya ukatili na mambo yasio na staha wanayofanyiwa na watu wazima.

Naye Ofisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia, Justine Basike aliwataka wadau wa maendeleo ya mtoto kushirikiana na jeshi hilo kuwabaini na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote wanaotuhumiwa kufanya matendo yanayowanyima watoto haki zao za msingi.

Kwa upande wake,  Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo, Leah Mwingira aliwataka watu wenye taarifa zinazohusu watoto kukosa haki zao kutozificha badala yake wazifikishe kwenye  ofisi yao au kwa timu za ulinzi na usalama wa mama na mtoto zilizoundwa katika ngazi ya kitongoji hadi wilaya.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz