Mtwara. Siku chache baada ya wanafunzi kuanza masomo imeelezwa kuwa mkoani Mtwara wanafunzi walioanza kidato cha kwanza ni 5,672 kati ya wanafunzi 22,810.
Kwa mujibu wa ofisi ya elimu Mkoa wa Mtwara, wanafunzi waliopangwa kuanza kidato cha kwanza katika shule mbalimbali wasichana walikuwa 12,066 na wavulana 10,744 lakini walioripoti hadi Januari 17, 2020 ni 5,672. Kati ya walioripoti wasichana ni 2,870 na wavulana 2,802.
Akizungumzia hali hiyo mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali amesema bado wanaendelea kuwahamasisha wazazi ili watoto wao waripoti shule.
Ofisa elimu taaluma Sekondari Wilaya ya Newala, Mussa Mussoma amesema wameweka mikakati kupita nyumba kwa nyumba, kwamba kuanzia jana idadi ya wanafunzi walioripoti imeongezeka.
Mussoma amesema kilimo cha kuhama sehemu moja hadi nyingine ni sababu ya wanafunzi kutofika shule.
“Eneo letu baadhi ya wazazi wanaenda Mkoa wa Lindi kulima ufuta wanashindwa kuhudumia watoto na wengine ni uvivu kwa sababu taarifa za ufaulu walipewa tangu Novemba 2019 lakini bado hajaripoti shule kuanza masomo,” amesema Mussoma
Pia Soma
- Mbunge Kenya kusota rumande kwa siku saba
- Mahakama yahoji upelelezi kesi ya Magoti wa LHRC
- Mahakama yaonya upande wa mashtaka kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Magufuli
Idadi ya halmashauri na walioripoti ni Masasi (549) Masasi mji (400), halmashauri ya wilaya ya Mtwara (333) manispaa ya Mtwara Mikindani (1,823), Halmashauri ya mji Nanyamba (268)
Halmashauri Nanyumbu (580) Newala (437) Newala mji (630) na Tandahimba (652)