Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 2,929  wa Lindi kupata elimu nje ya mfumo rasmi

13710c0cb9fb9f33ec3bda7e449b3832 Wanafunzi 2,929  wa Lindi kupata elimu nje ya mfumo rasmi

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI 2,929 ambao walifanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu mkoani Lindi na hawakufaulu watapangwa katika vituo vya ufundi stadi vilivyopo chini ya Halmashauri na wengine katika vituo vya Elimu ya Watu wazima vilivyo chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE) kupata elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi kwa kuchangia gharama kidogo.

Idadi hiyo ina wavulana 1,188 na wasichana 1,741 .

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu kilichofanyika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi chini ya uenyekiti wa Katibu Tawala, Rehema Madenge juzi.

Wanafunzi waliofaulu na wenye sifa za kujiunga kidato cha kwanza Januari, 2021 ambao jumla yao ni 15,944 (wavulana wakiwa 7,810 na wasichana 8,134), walichaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikali za bweni pamoja na za kutwa zilizopo mkoani idadi yao ni 15,944 sawa na asilimia 100 ambapo wavulana ni 7,810 sawa na asilimia 100 na wasichana ni 8,134 sawa na asilimia 100.

Hata hivyo kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo pamoja na wanafunzi wote kuchaguliwa, bado kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 36 katika sekondari za mkoa wa Lindi.

Lindi ilitegemea watoto 19,622 (Wavulana 9,397 na Wasichana 10,225) kufanya mitihani ambao ni sawa na asilimia 68.64 ya wanafunzi wote walioanza Darasa la Kwanza mwaka 2014 ambao jumla yao walikuwa 28,586 (Wavulana 14,476 na Wasichana 14,110).

Hata hivyo waliofanikiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) Septemba, 2020 walikuwa 19,387 (wavulana 9,260 na wasichana 10,127) sawa na asilimia 99.04 ya waliosajiliwa na watahiniwa ambao hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali ilikuwa 235 (wavulana 137 na wasichana 98) sawa na asilimia 1.43

Kwa takwimu zilizotolewa katika kikao hicho, watahiniwa waliosajiliwa mwaka 2020 wanawazidi wale waliosajiliwa mwaka 2019 kwa tofauti ya watahiniwa 1,161. Watahiniwa wasichana waliosajiliwa katika miaka yote miwili 2020 na 2019 walikuwa wengi kuliko watahiniwa wavulana.

Aidha, idadi ya watahiniwa waliofanya mtihani mwaka 2020 ni kubwa ukilinganisha na wale waliofanya mtihani mwaka 2019 kwa tofauti ya watahiniwa 1,190 na idadi ya watahiniwa wasiofanya mtihani mwaka 2020 ni ndogo ukilinganisha na ile ya waka 2019 kwa tofauti ya watahiniwa 29.

Akizungumzia matokeo hayo, Ofisa huyo wa elimu alisema mkoa wa Lindi umepata ufaulu wa asilimia 82.24 , ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.76 ukilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2019.

Aidha alisema katika taarifa ya NECTA, mkoa wa Lindi umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa mitatu iliyopandisha ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea imetajwa kuwa miongoni mwa halmashauri 10 zilizopandisha ufaulu kwa miaka tatu mfululizo.

“Katika matokeo ya shule ya msingi ya mwaka 2020, nafasi ya ufaulu ya mkoa wa Lindi kitaifa ni ya 14 kutoka ya 18 mwaka 2019 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania bara,” alisema Kayombo.

Aidha alisema wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani huu, kwanza kwa wavulana na wa kwanza kwa wasichana wametoka katika Halmashauri ya Nachingwea ambao ni Mzee Adamu (mvulana) kutoka Shule ya Msingi Muzdalifa Islamic (Nachingwea DC) mwenye jumla ya alama 239 na Beatrice Chengula (msichana) kutoka shule ya Msingi Namatula (Nachingwea DC) aliyepata alama 229.

Pia wanafunzi waliofanya vibaya katika matokeo hayo, kwa wavulana na wasichana ni Ramadhani Mwangalile kutoka shule ya Msingi Mtitimira Kilwa ambaye ana alama 2 kati ya 250.

Aidha Shule ya msingi Mtitimira (Kilwa) imejitokeza kuwa shule yenye ufaulu duni zaidi ndani ya mkoa kwa kuwa na wastani wa ufaulu wa 50.9 huku ikishika nafasi ya 492 kati ya 492 Kimkoa. Aidha, shule za Songomnara (Kilwa na Mputwa (Lindi DC) hazikufaulisha mwanafunzi hata mmoja.

Pamoja na matokeo hayo Ofisa elimu mkoa huyo alisema ugawaji wa nafasi katika shule za bweni umefanyika kwa kutumia uwiano wa wanafunzi waliofanya mtihani katika mkoa kwa kila Halmashauri dhidi ya waliofanya mtihani kimkoa kwa kuzingatia nafasi zilizotengwa na wizara yenye dhamana.

Alisema kwa Mwaka 2020, mkoa wa Lindi umetengewa nafasi za kidato cha kwanza 84 (wavulana 52 na wasichana 32) katika shule za bweni za serikali.

Aidha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais(TAMISEMI) amewapangia wanafunzi 34 wenye mahitaji maalumu kutoka mkoa wa Lindi shule za bweni na Kutwa.

Chanzo: habarileo.co.tz