Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 188 wapata ujauzito Mtwara mwaka 2018

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Watoto 188 wa shule za msingi na sekondari mkoani Mtwara wamekatishwa masomo baada ya kupata ujauzito kati ya Januari hadi Novemba 2018.

Takwimu zilizowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) leo na Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk Jilly Maleko zinaonyesha kati ya wanafunzi hao 150 ni kutoka shule za sekondari na 38 shule za msingi.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa wajumbe wa kikao, Dk Maleko amesema wilaya ya Tandahimba inaongoza kwa mimba 48 ambapo wanafunzi 20 toka shule za msingi walipata ujauzito huku sekondari wakiwa wanafunzi 28.

Ametaja wilaya inayofuata ni Masasi ambapo wana mimba 36, kati yao msingi wako sita na sekondari 30, Nanyumbu (25) msingi tatu na Sekondari 22, Manispaa ya Mtwara Mikindani ( 25) msingi mimba moja na sekondari 24.

“Halmashauri ya wilaya ya Newala mimba 18, mbili shule ya msingi na 16 sekondari, Mtwara kuna mimba 12, tatu shule za msingi na tisa shule za sekondari, Masasi Mji ziko 10 zote za sekondari.”

“Newala Mji mimba tisa, moja ya shule za msingi na nane za  shule za sekondari na Nanyamba Mji mimba tano ambazo mbili ni za shule za msingi na tatu sekondari” amesema Maleko.

Kufuatia taarifa hiyo Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameshauri kuundwa kwa mpango maalum ili kukabiliana na janga hilo.

“Sekretarieti ikakae waje  na mkakati madhubuti wa kupambana na hili tatizo, bila kufanya hivyo hii vita bado hatutaiweza kwa sababu bado takwimu ziko juu,” amesema Chikota.

Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amesema suala la mimba kwa wanafunzi pia linachangiwa na malezi kwa sababu wanafunzi wengine waliopata mimba wanaishi mjini na wako karibu na wazazi.

“Mtwara Mikindani kwa upande wa sekondari kuna mimba 24 na hapa ni mjini kwa maana watoto wanaamka kwao wanakwenda shule, kwa hiyo hizi mimba wamezipatia nyumbani tukiachana na hili mwenyekiti alilosema watoto wanakaa mbali na nyumbani kwao,” amesema Mwambe na Kuongeza

“Kwa Tandahimba tunazungumzia mimba 20 watoto wa shule za msingi, hawa nao wanatokea kwa wazazi wao kwa hiyo kuna suala la utamaduni na namna watu wanavyojali, ili tulikomeshe lazima tufuatilie kesi zilizopo kwa sababu ni za jinai,” amesema Mwambe

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema ili kuhakikisha mkoa unaondokana na tatizo hilo watakuja na mkakati ili kuwanusuru watoto.

“Sisi tunakimbilia mahakamani wanafunzi na wazazi wanakimbilia kuharibu ushahidi, mimi nimewahi kushauri sheria ibadilishwe imuwajibishe na mtoto wa kike,” amesema Byakanwa.

Amesema ni lazima kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike ili kujitambua kwa lengo la kupambana na mimba kwa wanafunzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz