Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 150 wakatisha shule kwa ujauzito

25053 UJAUZITO+PIC TanzaniaWeb

Fri, 2 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kongwa. Wanafunzi 150 wa sekondari wameacha masomo katika miaka minne wilayani hapa kuanzia mwaka 2015 hadi sasa kwa sababu ya ujauzito huku tatizo hilo likielezwa kuwa kubwa zaidi ya hapo.

Ofisa elimu vifaa na takwimu idara ya sekondari wilayani Kongwa, Selina Fundi alisema hiyo ni kwa wanafunzi walioripotiwa.

Fundi alitoa takwimu hizo akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Sejeli kwenye mradi wa Msichana Initiative ambao umeanzisha klabu mbalimbali za kutoa elimu.

Alisema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau, tatizo hilo limekuwa likiongezeka.

“Mwaka 2015 kulikuwa na mimba 27, mwaka 2016 zikawa 30; 2017 zikafika 48 na mwaka huu hadi sasa tuna taarifa ya mimba 45,” alisema Fundi.

Alisema kuna changamoto katika mapambano hayo kwani wazazi wamekuwa wakikubaliana wenyewe na kulipana bila kwenda mahakamani, hivyo kuvuruga ushahidi.

Hata hivyo, Fundi alisema katika matukio hayo zipo kesi ambazo zilipelekwa mahakamani na hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Alitaja sababu kubwa za mimba kuwa ni mila na desturi baada ya mtoto kufikia umri wa kuvunja ungo, wazazi wanaamini anapaswa kuolewa na hastahili kufanya mambo mengine.

Naye meneja miradi wa taasisi ya Msichana Initiative, Lineth Masala alisema wanalenga kutetea haki ya mtoto wa kike kwenye jamii na kuisaidia Serikali katika kutatua changamoto ambazo mtoto wa kike anakutana nazo.

Masala alisema tayari wamefungua klabu 11 katika shule za sekondari na tano za msingi ili kuwapatia elimu namna ya kujikinga na masuala hayo.

Mwalimu wa klabu ya wanafunzi wa shule hiyo, James Matupa alisema wapo kwenye jamii ambayo wazazi wengi hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa watoto wa kike na wa kiume katika kuwapa elimu ya masuala ya kijinsia.

Naye mwanafunzi Rosemery Jacob wa kidato cha pili, alitaja umaskini na ukosefu wa elimu kwa wazazi kama chanzo cha matatizo hayo hali inayosababisha wanafunzi kujiingiza kwenye uhusiano wa mapenzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz