Arusha. Wanafunzi 11,200 katika halmashauri ya Jiji la Arusha nchini Tanzania wanatarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi itakayofanyika Jumatano na Alhamisi wiki hii.
Ofisa Elimu Msingi wa jiji hilo, Omari Kwesiga amesema hayo leo Jumatatu Septemba 9,2019 wakati akizungumza na Mwananchi juu ya maandalizi ya mitihani hiyo ambayo inahitimisha safari ya miaka saba ya wanafunzi hao.
Amesema kati ya wanafunzi hao wavulana ni 5,405 na wasichana ni 5,795 kutoka Shule 130 kati ya hizo shule za serikali ni 46 na binafsi ni 84.
“Tumejiandaa vizuri sana wanafunzi wetu wamefanya mitihani ya majaribio ya kutosha na jiji limefanya vizuri kwenye mtihani wa mwisho na kuziacha halmashauri zingine katika mkoa wetu kwa mbali, hivyo tunatarajia kufanya vizuri zaidi ya mwaka jana,” amesema Kwesiga
Kuhusu iwapo wamiliki wa shule binafsi kuwazuia wanafunzi wao kufanya mitihani kabla ya kumaliza ada na michango mingine amesema hakuna mwenye mamlaka ya kuwazuia wanafunzi kufanya mitihani kwa sababu ya kutokukamilisha ada au michango .
Amesema kama suala hilo lipo unapaswa kufanyika utaratibu kati ya mzazi na mmiliki wa shule namna ya kukamilisha malipo bila kumzuia mwanafunzi kufanya mitihani yake na kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria.
Pia Soma
- VIDEO: Mmiliki wa baa Dar abanwa na Waziri Lugola, aishiwa nguvu
- Shule za Atlas zafanya maombi kuelekea mtihani darasa la saba
- VIDEO: Udom wazungumzia matokeo ya wanafunzi 8,500 kuzuiwa