Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 100 wasoma chumba kimoja Dodoma

81810700b59392cf28534e9f0991d75e Wanafunzi 100 wasoma chumba kimoja Dodoma

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHULE ya Msingi Michese iliyopo kata ya Mkonze, jijini Dodoma inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa, hali inayofanya wanafunzi zaidi ya 100 kusomea katika chumba kimoja na kuhatarisha usalama wa afya zao.

Hali hiyo ilibainika juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kufanya ziara katika shule hiyo ili kujionea maendeleo ya elimu akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Baada ya kushuhudia hali hiyo, Mtaka alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Jjiji la Dodoma, Joseph Mafuru kushughulikia uhaba wa vyumba vya madarasa haraka, huku akieleza kuwa tayari serikali ilishapitisha bajeti ya elimu hivyo katika fedha watakazopokea wahakikishe wanaifikia shule hiyo.

"Ili kuwe na ufaulu mzuri lazima miundombinu ya elimu iwe mizuri hasa ikizingatiwa kuna ugonjwa wa covid-19 na wanafunzi wengine kukaa chini kwa ukosefu wa madawati, hii kwetu ni aibu," alisema.

Alisema licha ya shule hiyo kuwa katikati ya Jiji la Dodoma, haina hadhi na kusisitiza wahusika kukarabati miundombinu ya majengo na nyumba za walimu, pamoja na ujenzi wa vyoo vya walimu na huduma za maji.

"Katika karne hii kweli bado kuna shule ambazo wanafunzi wanakaa chini!, lazima sisi kama viongozi tuzitendee haki nafasi zetu katika kutoa huduma hasa katika masuala ya elimu ili watoto wetu wasome kwa ari," alisema Mtaka.

Aidha, aliwataka wazazi kuacha kuwapa watoto majukumu mengi ya kazi za nyumbani, badala yake kuwaachia muda mrefu wakiwa nyumbani wapate muda mwingi wa kujisomea kwa kuwa elimu ndio msingi wa maisha yao.

Awali, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Michese, Sizya Wiliam alisema shule hiyo ina wanafunzi 1,850, vyumba vya madarasa tisa na upungufu wa madawati 100.

Alisema pia shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyoo vya walimu ambapo kwa sasa wanajisaidia kwa kutumia vyoo vya wanafunzi na kwa majirani wa shule hiyo.

"Ni jambo la aibu kwetu, shule yetu inakabiliwa na changamoto nyingi kama unavyoona mrundikano katika vyumba vya madarasa na pia tuna uhaba wa madawati, hata hivi vyumba vya madarasa tisa vilivyopo ni chakavu kabisa.”

"Pia tuna uhaba wa walimu maana nina walimu 30, kati yao mmoja ni wa kujitolea, hivyo walimu waliopo hawaendani na ikama ya wanafunzi waliopo jambo linafanya kushuka kwa ufaulu shuleni hapa," alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Shekimweri alisema kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa vilivyopo, atachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kufyatua matofali ya kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz