Jumla ya wanafunzi, 1,776 wa Shule ya Msingi Mabonde jijini Mbeya, wanatumia matundu 16 ya vyoo shuleni hapo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Raphael George ambaye ni mkuu wa shule hiyo, idadi hiyo inajuisha wakiwepo wasichana 898 na kwamba kati ya matundu hayo, nane hutumiwa na wanafunzi wa kike.
George amesema leo Ijumaa Julai 14, 2023 mara baada ha Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini Dk Tulia Ackson kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya elimu hususan ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kalobe Jijini hapa, ambavyo vilibomoka mwaka jana.
George amesema ili kukidhi idadi ya matundu ya vyoo yanayotakiwa, shule hiyo itahitaji jumla ya matundu matunda 36 na hivyo kukidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi katika shule hiyo.
“…ujio wako uwenda ukawa msaada mkubwa kwetu na kunusuru afya za watoto wetu, hata hayo matundu 16 yaliyopo yana hali mbaya ambayo yanahitaji kufanyiwa matengenezo ili kukidhi vigezo kwa matumizi ya binadamu,” amesema Mwalimu Geogre.
Mkuu huyo wa shule amemueleza Dk Tulia kuwa changamoto zingine zinahusu miundombinu ya madarasa ambavyo ni chakavu, na upungufu wa madawati 140 huku yaliyopo ni 560 pekee.
Kwa upande wake, mbunge huyo ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri, amesema lengo la ziara yake ilikuwa kutembelea miradi ya elimu kwenye shule za msingi na sekondari jijini hapa ambazo zilizopokea fedha mradi wa boost.
“Nimeona na kusikia changamoto ya uchakavu wa vyoo natoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya vyoo na madawati 140 sambamba na msukumo kwa Jiji kutoa kiasi cha Sh20 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa matundu ya vyoo 23 katika Shule ya Sekondari Kalobe,” amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kalobe, Ally Bromela ameshukuru ujio wa mbunge wao kwamba atakuwa msaada wa kusukuma jiji kutoa fedha kukamilisha mradi wa matundu ya vyoo shule ya Sekondari Kalobe kwani yeye amefuatilia bila mafanikio.
Awali Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema kuwa watashirikiana na mbunge kuhakikisha hakuna mahala patakapo kwama katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuweka msukumo kwenye maeneo yenye changamoto.
“Halmashauri itaongezeza nguvu kuboresha miundombinu ya elimu kwani Spika na Mbunge wetu amekuwa msaada mkubwa, mambo ambayo yalistahili sisi tufanye anafanya ikiwepo ujenzi wa matundu ya vyoo vyumba vya madarasa na mabweni kwa wanafunzi wa kike,” amesema.