Kero ya uwepo wa vikundi vya vijana vinavyofanya vitendo vya kihalifu vijulikanavyo kama damu chafu au maarufu 'Panya rodi, imebuka katika mkutano wa hadhara wa Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Paul Makonda uliofanyika Mpanda mkoani Katavi.
Katika mkutano huo uliofanyika jana Jumapili Februari 4, 2024 katika uwanja wa Kashaulili, baadhi ya wananchi wenye mabango walimuomba kiongozi huyo kuwasaidia kutatua changamoto vikundi vya damu chafu, ambavyo vimekuwa tishio katika Manispaa ya Mpanda.
Hata hivyo, akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani alikiri uwepo wa vikundi hivyo, lakini polisi wamefanikiwa kuvidhibiti kwa asilimia 90, huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano zaidi.