Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamkumbuka alivyoshawishi watanzania kurejea tiba asili

471490501095b04ddd7fae46604ecf2e Wamkumbuka alivyoshawishi watanzania kurejea tiba asili

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAALAMU wa tiba asili Manispaa ya Shinyanga wamemlilia Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kwa kusema alisisitiza matumizi ya dawa za asili hasa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19.

Pia wameiomba serikali kufanya utafiti wa miti ya asili kutokana na kuanza kutoweka huku wakiomba kupatiwa mashamba ili waweze kupanda miti ya dawa za asili ambayo itasaidia kwa tiba ya magonjwa mbalimbali.

Mtaalamu wa tiba za asili Manispaa ya Shinyanga, Mrisho Kuhangaika aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Magufuli kuthamini tiba mbadala na kuwasisitiza watanzania kutumia tiba hizo.

Kuhangaika ambaye pia ni mfanyabiashara alisema Magufuli alikuwa ana mchango mkubwa katika kuwahimiza watanzania kutumia dawa za asili kukabiliana na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mfumo wa hewa.

Mtaalamu mwingine wa tiba asili, Hassan Karim alisema ni wakati sasa umefika kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuinusuru miti ya asili isiendelee kupotea kwa kuwawezesha kupata mashamba ya kupanda miti ya asili ya dawa.

Kiongozi wa wataalamu wa tiba mbadala stendi ya zamani Shinyanga, Mussa Kambala alisema kifo cha Magufuli kimewashitua na kupoteza matumaini kwani ndoto zao hawajui kama zitatimia za kusaidia watanzania wengi.

"Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuthamini mchango unaotolewa na wataalamu wa tiba mbadala na kuendeleza yote ambayo alikuwa akifanya Magufuli kuwasaidia wanyonge,"alisema Kambala.

Kambala alisema Magufuli alikuwa akiwasisitiza watanzania kutumia dawa za tiba za asili kutibu magonjwa mbalimbali pamoja na kujifukiza ili kusaidia kukabiliana na homa kali ya mapafu ambayo inatikisa dunia kwa sasa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz