Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamisionari wanavyoing’arisha Ndanda kwa umeme wa uhakika

56073 PIC+UMEME

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Nishati ya umeme ni kati ya nyenzo muhimu ya kiuchumi inayorahisisha huduma za maendeleo ya kijamii.

Hata utekelezaji wa dira ya Mendeleo ya Taifa 2025 ili kufikia nchi yenye uchumi wa kati kupitia maendeleo ya sekta ya viwanda inategemea zaidi upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa nishati, kuna vyanzo vingi vya umeme, lakini vilivyo na uhakika inaelezwa ni nishati jadidifu.

Licha ya urahisi, aina hii ya nishati pia ni endelevu kwa sababu hutokana na mionzi ya jua, maporomoko ya maji, upepo na kinyesi cha wanyama.

Kwa wakazi wa wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, jina la Wamisionari wa Wabenedikitine Abasia ya Ndanda ni maarufu siyo tu kwa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii kama vile afya, elimu na uchumi. Yote yanawezekana kwa wamisionari hao kwa sababu ya nishati jadidifu kwa uhakika wa umememaji.

Watumishi hao wa kiroho wanazalisha nishati ya umeme kwa kutumia maji. Umeme huo licha ya kutumika katika hospitali ya Rufaa ya Mt Benedikto Ndanda, pia ni tegemeo kwa matumizi katika karakana na chuo cha ufundi na uuguzi vilivyomo katika eneo hilo maarufu la Ndanda.

Mwalimu wa umeme katika chuo cha Ufundi Ndanda, Mussa Mwambe anasema kwa siku wanazalisha kilowati 286 ambazo hutumiwa na zaidi ya taasisi tano zilizopo eneo hilo.

“Umeme tunaozalisha ni kwa ajili ya matumizi ya taasisi zilizo chini ya Abasia ya Ndanda, kama karakana, hospitali, chuo cha ufundi Ndanda, chuo cha uuguzi Ndanda na Jumuiya mbili kubwa za watawa Tutzing na Ndolo. Kila kitengo au Jumuiya ina mita yake kwa ajili ya huduma na kulipia gharama ya uendeshaji,” anasema Mwambe.

Anabainisha maji wanayotumia kuzalisha umeme ni ya chemchemi ambayo huelekezwa lilipo bwawa na kupelekwa kwenye mitambo kwa ajili ya kuzalisha umememaji.

“Maji yanatoka kwenye bwawa yanakuja kusukuma mitambo na kuzalisha umeme ambao unatumika katika taasisi zote zilizo chini ya Abasia ya Ndanda,” anasema.

Faida zipatikanazo

Anasema shughuli zao zinafanyika wakati wote kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika.

“Shughuli zetu zote zinaenda hakuna tunapokwama, na hatusumbuani na mtu yeyote. Kwa sasa mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko uwezo wetu,” anasema Mwambe na kuogeza;

“Taasisi zote zilizo chini ya Abasia ya Ndanda kama hospitali, vyuo na karakana ndio wateja wetu na hakuna anayemhudumia mwenzake bila gharama, mtu wa shule akienda hospitali atalipia hivyo hivyo kwa mtu wa hospitali akihitaji huduma ya umeme lazima alipie,” anasema

Anaeleza mambo ya msingi kuzingatia wakati wa kuzalisha nishati jadidifu ya umememaji ni uhakika wa upatikanaji wa maji ya kutosha.

Mganga mkuu wa hospitali ya Rufaa, Mt Benedikto Dk Stanslaus Wambyakale anasema wakati wa utoaji wa huduma wanajivunia upatikanaji wa umeme wakati wote. Dk Wambyakale anasema faida wanazozipata kutokana na matumizi ya nishati jadidifu ni kupata umeme saa kwa 24. Anasema wanapotoa huduma wanakuwa hawana wasiwasi na umeme hasa katika upasuaji na huduma nyinginezo zinazohitaji umeme.

“Umeme ni wa uhakika, haukatiki na una nguvu ya kutosha kuendesha shughuli zetu ukizingatia kitengo cha X-ray kinatumia sana umeme huku maabara vitu vyake takribani vyote vikihitaji umeme,” anasema Dk Wambyakale.

Ofisa utawala wa Abasia ya Ndanda, Padre Alfons Holela anasema waliamua kutumia nishat jadidifu ya umememaji baada ya kutokuwa kwenye gridi ya Taifa na kutumia teknolojia kuzalisha umememaji kwa matumizi ya taasisi hiyo kubwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz