Wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wametakiwa kusajili vituo hivyo sambamba na kuboresha mazingira yanayofaa kwaajili ya watoto hao.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wakutambulisha programu jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (MMMAM) Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Mtwara, Mikindani Felista Kyando alisema kuwa vituo vingi vinahitaji maboresho makubwa vina hali mbaya.
“Sisi hatuna mamlaka ya kufunga vituo hivyo mwenye mamlaka ni Katibu Mkuu, vituo vingi havikidhi vigezo vya kupata usajili lakini usajili ni bure hakuna gharama wanazotozwa,” amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Sefty Alliance TASA, John Daniel alisema kuwa wamiliki wa vituo vingi wanaangalia pesa bila kujali ulinzi na usalama hali ambayo inapelekea mtoto kuwa katika mazingira yasiyofaa.
“Wamiliki wengi wanaangalia pesa ila hawaangalii manufaa ya watoto hali ambayo inapelekea watoto kufanyiwa ukatili wa kijinsia naamini kupitia mpango huu utasaidia kuboresha vituo vya kulelea watoto mchana” alisema Daniel.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Nanjiva Nzunda alisema kuwa ulinzi na salama wa mtoto unatakiwa kupewa kipaumbele ndani ya mkoa huo.
“Tupate ripoti ili tuwajue ambao bado sio sawa kukaa na vituo ambavyo havijasajiliwa alafu usajili ni bure inawezekanaje Manispaa viwepo vituo 91 alafu vituo 51 tu ndio visajiliwe nendeni mkafanye kazi na mchukue hatua,” alisema Nzunda.
Kwa upande wake Meneja wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya KIMASI ambayo ndio kiongozi mradi wa MMMAM ikishrikiana na mtandao wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto Tanzania (TECDEN), Torai Kibiti alisema kuwa programu hiyo inaangalia malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Zipo taasisi ambazo hazijasajiliwa lakini zina lea watoto sio jambo zuri ni vizuri katika lile eneo la kuimarisha mifumo tukaanza na usajili na kutoa elimu kwanini zisajili na kuwaambia umuhimu wa kusajili vituo hivyo,” alisema Kibiti.
Pia, Mwezeshaji wa Elimu ya Sayansi ya Malezi Makuzi, Edwerd Bishara amesema kuwa wanatekeleza programu ya mtoto kwanza kwenye mpango wa taifa wa makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto.
“Sisi kama wadau lengo letu kubwa ni kufundisha wadau ili waweze kuhitimisha na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika programu hiyo lengo kubwa ni kuona mtoto wa miaka 0-8 anapitia misingi bora na imara kuanzia kwenye familia,” alisema Biashara.