Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamiliki nyumba 80 walipwa fidia kupisha ujenzi ‘airport’ Musoma, mmoja agoma

Nyumba Pic Data Wamiliki nyumba 80 walipwa fidia kupisha ujenzi ‘airport’ Musoma, mmoja agoma

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wamiliki wa nyumba 80 katika eneo lililopo karibu na Uwanja wa Ndege Musoma mkoani Mara wamelipwa fidia ya jumla ya Sh3.953 bilioni kwaajili ya kupisha ujenzi wa uwanja huo unaotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Hata hivyo mmiliki wa nyumba moja amegoma kupokea fidia kwa madai kuwa thamani ya nyumba yake hailingani na fedha ambazo alitakiwa kulipwa na serikali.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa uwanja huo leo Novemba 17, 2021 kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya aliyefanya ziara kukagua mradi huo, kaimu meneja wa Wakala wa Barabara nchini ( Tanroads) mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwakani.

Amesema kuwa ujenzi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh35 bilioni hivi sasa umefikia asilimia 8 na kwamba tayari mkandarasi anayetekeleza mradi huo amekwishalipwa Sh3.078 bilioni kama malipo ya awali.

"Mkandarsi wa mradi huu amekwishalipwa malipo ya awali ya Sh3.078 bilioni na ujenzi umeanza mwezi Septemba mwaka huu licha ya mkataba kusainiwa mwezi Aprili mwaka huu" amesema Maribe

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya ameagiza Tanroads kusimamia tathmini upya ili mtu huyo aliyegoma kupokea fidia aweze kulipwa ili kupisha mradi huo.

Amesema kuwa Serikali haipo tayari kuona mtu ananyimwa haki yake lakini pia mtu huyo asiwe kikwazo cha kuendelea kwa mradi huo kwa wakati hivyo ni vema Tanroads kwa kushirikiana na mthamini mkuu wa Serikali ikahakikisha kuwa mtu huyo analipwa ili asiathiri maendeleo ya mradi.

"Hatuwezi kumuonea mwananchi ni lazima haki yake ipatikane hivyo naagiza muwasiliane na vyombo vinavyohusika na tathmini ili hatua zichukuliwe za haraka ili mtu huyu aweze kupisha na kuepusha mkandarasi kukutana na kikwazo wakati akiendelea na kazi" amesema

Pia ameagiza Tanroads kuhakikisha kuwa wanamsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa baada ya ujenzi wa mradi huo kuchelewa kuanza kwa wakati na kuagiza mkandarasi kuongeza idadi ya wafanyakazi na muda wa kufanya kazi ili kufidia muda uliopotea kabla ya ujenzi kuanza.

Serikali imelipa fidia ya zaidi ya Sh3.953 bilioni kwa wamiliki wa nyumba zilizopo kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma mkoani Mara huku mmiliki mmoja akigoma kupokea fidia hiyo kwa madai kuwa fidia hailingani na thamani ya nyumba yake.

Chanzo: mwananchidigital