Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamiliki daladala Mwanza waukana mgomo

Waendesha Daladala Mwanza Wameweka Mgomo Kwa Muda Usiojulikana.jpeg Wamiliki daladala Mwanza waukana mgomo

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umoja wa Madereva na Makondakta Mkoa wa Mwanza, (Mwaredda) na Chama cha Wamiliki wa daladala mkoani humo (MTA), wamekanusha kuwa na taarifa ya uwepo wa mgomo wa daladala mkoani humo.

Madereva na makondakta mkoani humo leo Jumatatu Machi 11, 2024, wamesitisha usafirishaji wa abiria jambo lililowalazimu wananchi kutumia pikipiki za matairi matatu “bajaji’ na zile za kubebea mizigo, huku wakitozwa nauli ya Sh2,000 katika eneo ambalo kwenye daladala wanalipia Sh600.

Akizungumza na Mwananchi, Mkazi wa Butimba jijini humo, Tausi Mussa ambaye ni mfanyabiashara wa mbogamboga amesema awali kutoka nyumbani kwake hadi Buhongwa alikuwa analipa Sh600, lakini kutokana na mgomo huo amelipia Sh2,000 kwenye bajaji.

Kondakta katika gari inayotoa huduma kati ya Mwanza Mjini hadi Buhongwa, Gabriel Stanslaus amesema utitiri wa bajaji umesababisha biashara ya daladala kudorora, kwa kile wanachodai kwamba bajaji hizo zinawaibia wateja ‘kuwaosha’ huku Mwenyekiti wa MTA, Yusuph Lupilya akisema hawakuwa na taarifa ya kuwepo mgomo huo leo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya wilaya zilizoathiriwa na mgomo huo, ametoa saa 2 kuanzia Saa 6:30 mchana, madereva walioegesha daladala zao kuzirejesha na kuanza kutoa huduma mara moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live