Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamachinga wavamia ofisi ya mkuu wa wilaya

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Wafanyabiashara wadogo katika Manispaa ya Tabora juzi wamevamia ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Tabora kutaka kujua hatima ya mgawo wa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga.

Wakizungumza na Mwananchi katika viunga vya ofisi hizo, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema wemefikia uamuzi huo baada ya kuona utaratibu wa kuwagawia vitambulisho hivyo haujawekwa wazi huku wenzao wa maeneo mengine wakiendelea kugawiwa.

“Tumesubiri kwa muda mrefu kupata utaratibu utakaotumika kugawa vitambulisho sasa tumechoka, tumekuja hapa kujua kulikoni Tabora hali ni kimya wakati maeneo mengine tunashuhudia wakigaiwa,” alisema Sikudhani Seif, mfanyabiashara wa mtaa wa Kanyenye.

Mfanyabiashara mwingine, Said Idi kutoka mtaa wa Chekuwa alisema kwamba wanahitaji vitambulisho hivyo ili kuondokana na usumbufu kutoka kwa askari wa manispaa na mamlaka nyingine za halmashauri.

Akizungumzia suala hilo, mkuu wa wilaya ya Tabora, Eric Komanya alisema kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na watendaji kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, kata na halmashauri inakamilisha mchakato wa kuwatambua wafanyabiashara wenye sifa za kugaiwa vitambulisho hivyo ili kuhakikisha haviangukii mikononi mwa wasiostahili.

“Tumetoa mafunzo maalum kwa wafanyabiashara tukishirikiana na TRA, kinachofuata ni wafanyabiashara hao kujiandikisha na kujaza fomu maalum katika maeneo yao ambazo zitawasilishwa ofisi ya mkuu wa wilaya kwa uhakiki kabla ya kugaiwa,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz