SERIKALI imesema inakuja na mpango mkakati wa kuondoa adha ya wamachinga kwa kuanza kuwaondoa walioweka vibanda juu ya mifereji ya maji, katika njia za wapiti kwa miguu, hifadhi za barabara na mbele ya maeneo ya taasisi za umma kama mashuleni.
Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alipokutana na kufanya majadiliano na viongozi wa wafanyabiashara jijini hapo.
Amesema mpango huo haunalengo la kuwaondoa wamachinga ila dhumuni lao ni kuona kuwa wafanyabiashara, mamalishe na babalishe wanaendeleza shuhuli zao za kujiingizia kipato lakini katika maeneo mazuri waliyopangwa bila kuathiri shuhuli za watu wengine.
“Tumekuwa katika mkutano wetu wa pamoja na naamini wote tukiwa na uelewa wa pamoja suala hili la kuwapanga wamachinga katika mkoa wa Dar es Salaam litaenda vizuri na litakuwa na manufaa kwa wamachinga wenyewe, serikali na wadau wengine ambao kwa namna moja ama nyingine tulipita katika kipindi ambacho kulikua na mkanganyiko,” amesema Makalla.
Ameongeza kwa kuwaomba wamachinga kutoa ushirikiano katika wilaya na katika mikutano kama walivyokubaliana na kesho ‘leo’ kutakuwa na uzinduzi rasmi wa mpango wa mkoa huo kuonesha namna walivyokuwa wamejipanga katika kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa biashara mkoani hapo.
Amesema mpango huo utaainisha maeneo mbalimbali ya kuwapeleka wamachinga, pamoja na kuweka uwezekano wa kufunga baadhi ya mitaa kwa muda ili itumike kuendesha biashara, na alieleza kuwa mamlaka hayo yatakuwa chini ya uongozi wa halmashauri, huku ofisi yake ikibaki kama mratibu mkuu wa zoezi hilo.
Aidha maandalizi hayo yataenda sambamba na uzinduzi wa madawati ya wamachinga katika kila halmashauri yatakayotumika kusikiliza kero zao na kujua namna ya kuwapanga, kujua na kupata kanzi data itakayotumika katika kuweka mpangilio mzuri wa wafanyabiashara katika eneo husika.
“Naamini kabisa kuwa Dar es Salaam yenye kufanya biashara vizuri kama watu watapangwa inawezekana,” amesema Makalla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga, Steven Lusinde amemshukuru mkuu wa mkoa huo kwa kuwashirikisha katika suala la upangwaji wao kwani walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo ya namna bora ya kufanikisha mpango huo.
“Tumefurahi kwani hicho kilikuwa kilio chetu kikubwa kuwa katika mpango huo sisi ambao ndo walengwa lazima tushirikishe katika mijadala inayotuhusi, hivyo nimshukuru mkuu wa mkoa, na tutakaa na wakuu wa wilaya kuona namna ya kutekeleza maagizo yaliyotolewa,” amesema Lusinde.