Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamachinga Dar wadaiwa kuvamia eneo la kanisa

Wamachingapic Makamu Askofu kanisa la Orthodox jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba

Sun, 14 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wamachinga jijini Dar es Salaam waliohamishwa eneo la Mbuyuni kata ya Wazo Wilaya ya Kinondoni wanadaiwa kuvamia eneo la kanisa la Orthodox na kuanza kufanya biashara jambo lililolalamikiwa na uongozi wa kanisa hilo.

Kundi la wamchinga zaidi ya 200 wamevamia eneo hilo wakidai kuwa ni la wazi linamilikiwa na Serikali hivyo wanaenda hapo kufanya biashara zao baada ya kufukuzwa barabarani.

Makamu Askofu wa kanisa hilo jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba amesema kuvamia kwa wamachinga hao katika eneo lao kumesababisha baadhi ya shughuli za kanisa kusimama.

Amesema tayari wameshatoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za mtaa na wilaya ambao uliwarudishia majibu kuwa eneo la kanisa si eneo sehemu ya afanyabiashara hivyo wavamizi wanapaswa kuondoka kupisha shughuli za kanisa kuendelea.

“Wakati Serikali inafanya oparesheni ya kuwaondoa wamachinga barabarani ndipo hawa wa eneo la Mbuyuni wakavamia eneo letu hili la kanisa na kukwamisha shughuli zingine kuweza kuendelea,” amesema

Paroko wa kanisa hilo, Padri Frumentios Msuri amesema kanisa hilo la Bikiria la Maria lilijengwa mwaka 1939 na tangu hapo Watanzania, Wagiriki na watu wa aina mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusali lakini baada ya vurugu hizo wamelazimika kusali Upanga.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wamachinga hao, Kizito Ponsiano amesema wafanyabishara hao hawafanyi biashara zao katika eneo la kanisa na kusisitiza kuwa eneo hilo sio lote ni mali ya kanisa.

Hata hivyo amesema wanauomba uongozi wa kanisa hilo kuwapatia vielelezo vinavyoonesha kuwa eneo hilo ni mali yao na kwamba wakiviona na kujiridhisha wataondoka na kutafuta eneo jingine.

Akijibu madai hayo, mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mbuyuni Salasala, Robart Masawe amesema katika eneo lake wafanyabiashara wamepangiwa eneo la Benako ambalo lina mgogoro na eneo la Kisanga ambalo halina choo kwa sasa.

“Diwani anapambana sasa hivi ili kupatikane choo, tukimaliza kujenga wamachinga hawa watatolewa na kwenda kupangwa katika eneo hilo wala hakuna tatizo,” amesema

Hata hivyo Masawa amesema eneo waliopo wafanyabiashara hao limejitenga kabisa na kanisa hilo, na kuongeza kuwa mgogoro huo ulipofikia wanaliomba kanisa kuleta vielelezo vyao.

Chanzo: mwananchidigital