Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walipuka kwa shangwe baada ya kukabidhiwa leseni ya uchimbaji

65738 Shangwee+pic

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga.  Vifijo vigelegele na nderemo vimerindima kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu uliopo katika Kijiji cha Mwakitolyo , Shinyanga vijijini baada ya kuwasili kwa Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Biteko amefanya ziara hiyo leo Ijumaa Julai 5, 2019 katika mgodi huo ili kukabidhi leseni za uchimbaji madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo kwenye eneo lililokuwa linamilikiwa na kampuni ya Pangea Minerals.

Awali, Rais John Magufuli aliamuru leseni ya kampuni hiyo ifutwe na kukabidhiwa kwa wachimbaji wadogo.

Waziri Biteko amepokelewa na umati wa wachimbaji wadogo waliokusanyika kumlaki kwa mchakamchaka huku wakiimba wimbo uliotaja majina ya Rais Magufuli na waziri Biteko.

Akizungumza na wachimbaji hao, Waziri Biteko  amesema atafurahi kusikia baada ya miezi mitatu ulipaji mapato ya Serikali unaongezeka katika eneo hilo.

 “Ndugu zangu naona aibu sana kusikia taarifa ya mapato kutoka eneo hili, inasomeka sifuri, nifurahisheni na mimi kama mnavyo furahi ninyi hii leo, mkilipa  mapato ya Serikali kama mlivyonipokea kwa shangwe, nifanyeni nami kuwa mwenye furaha na shangwe kwa kulipa mapato ya Serikali,” amesema Biteko na kuongeza;

Pia Soma

“Kauzeni madini yenu kwenye soko halali, acheni kutorosha madini na nataka nitakapofika awamu nyingine namba ziwe zinasomeka tofauti na sasa.”

Katika kazi hiyo ya kukabidhi leseni, kilio cha Biteko ni kuwaomba wachimbaji wadogo kuzingatia taratibu na matakwa ya sheria ya uuzwaji wa madini kwenye masoko, kutotorosha madini na kulipa maduhuli ya Serikali.

Amesema Rais Magufuli anawajali wachimbaji wadogo, ndiyo maana hata kwenye orodha ya Makamishna wa Tume ya Madini, Mtendaji mkuu wa chama cha wachimbaji wadogo ni miongoni mwa makamishna aliyeteuliwa kuwasilisha masuala ya wachimbaji wadogo.

Awali, Kiongozi  wa Wachimbaji wadogo nchini (FEMATA) John Bina alisema wanachoahidi ni kutekeleza agizo la ulipaji wa mapato.

 “Waziri nikuombe leo tukutume, tufikishie salamu za shukrani kwa Rais Magufuli, kamwambie tumefurahi na tunakushuru kwa uamuzi wake, sisi tuna ahidi kutekeleza yote yanayotupasa kutekeleza,” amesema Bina.

Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Profesa  Shukrani Manya amewaomba wachimbaji hao kuzingatia masharti ya leseni waliyopewa kwa kulipa asilimia saba kati ya 100 ya wanachozalisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz